Mapapa wa mihadarati kushtakiwa Marekani

11Apr 2017
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mapapa wa mihadarati kushtakiwa Marekani

WAZIRI wa Katiba na Sheria, amewasilisha maombi mahakamani akitaka kibali cha kuwasafirisha wafanyabiashara watatu wakubwa wa mihadarati, akiwamo Ali Haji, maarufu kama Chikuba, kwenda nchini Marekani kujibu tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi (wa pili kushoto) picha na maktaba.

Maombi hayo yaliwasilishwa jana na Jamhuri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi Cyprian Mkeha. Mbali na Shikuba watuhumiwa wengine ni Idd Mfuru na Tiko Emmanuel.

Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Veronika Matikila alidai kuwa upande wa Jamhuri unawasilisha maombi matatu tofauti, dhidi ya walalamikiwa kwamba waziri anaomba mahakama itoe kibali cha kusafirishwa kwenda nchini Marekani kujibu mashtaka ya kujihusisha na dawa za kulevya.

Jamhuri ilidai kuwa maombi hayo yamewasilishwa kupitia Sheria ya Usafirishaji wa Wahalifu, sura ya 368, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 chini ya kifungu cha 5(1) cha sheria hiyo.

Pia, Jamhuri ilidai, maombi hayo yamewasilishwa chini ya kifungu cha 11(a) cha Sheria ya Usimamizi wa Mashtaka ya mwaka 2008 na cha 392 (A) cha sheria.

Upande wa Jamhuri unaomba maombi hayo yasikilizwe kwa kuwasilisha hoja kwa njia ya mdomo.

“Ombi letu mahakama isikilize ushahidi na itoe amri ya kuwahifadhi walalamikiwa ndani (mahabusu) wakati akisubiri kibali cha waziri cha kumsafirisha nje ya nchi kwenda kusikiliza mashtaka yake,” alidai Kakolaki.

Akijibu hoja za Jamhuri, upande wa walalamikiwa ukiongozwa na Mawakili Majura Magafu na Hudson Ndusyepo, ulidai kuwa umesikia maombi hayo.

“Kumchukua raia wako kumpeleka nchi nyingine ni suala zito na kwamba mashtaka hayo yalipaswa kuletwa mbele yake ili walalamikiwa waweze kujua kiini cha maombi hayo,” alidai Magafu.

Alidai kuwa upande wa walalamikiwa unaomba muda kwa ajili ya kupitia maombi hayo ili waweze kujibu na waweze kuwawakilisha vizuri wateja wao.

Hakimu Mkeha alisema maombi hayo yatasikilizwa leo.

Chikuba (50 alikamtwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Machi, 2014 baada ya kuwindwa kwa miaka miwili kabla ya kuhamishiwa mkoani Lindi.

Anatuhumiwa kuwa kiongozi wa genge la wauza madawa ya kulevya lenye makao yake Afrika Mashariki lakini likiwa na uhusiano wa kibiashara mpaka China, Brazil, Canada, Japan, Marekani na Uingereza.​

Habari Kubwa