Mapendekezo sheria watu kujipima ukimwi kupitishwa bungeni

12Nov 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Mapendekezo sheria watu kujipima ukimwi kupitishwa bungeni

SERIKALI imesema mwishoni mwa wiki hii bunge linatarajia kupitisha mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ili watu waweze kujipima wenyewe virusi vya ukimwi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalim

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akifungua semina elekezi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), kwa wasanii mbalimbali iliyoandaliwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin William Mkapa.

Waziri alisema awali sheria ilikuwa hairuhusu kujipima, hivyo sheria itakapopitishwa watu wataweza kujipima wenyewe.

Alisema kuna marekebusho ya sheria yamepelekwa bungeni  ili watu waweze kujipima wenyewe.

"Sheria hiyo ya ukimwi inasema mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 hawezi kwenda kupima ukimwi bila ridhaa ya wazazi wake," alisema.

Waziri Ummy alisema  kila Watanzania 100, watanzania 80 wanafahamu kuhusu virusi vya ukimwi na ukimwi.

Alisema Tanzania imejiwekea malengo ya kutokomeza ukimwi ifikapo 2030 na  watu Milioni 1.4  nchini wanaishi na virusi vya ukimwi na kuna changamoto kubwa ya baadhi ya watu hawafahamu hali zao.

“Nawaomba sana katika kazi zenu za Sanaa kwenye nyimbo maigizo filamu Sanaa za maonyesho katika kuhamasishana. Kwani Katika watu 100 wanaoishi na virusi vya ukimwi ni watu 62 tanzania ambao wanafahamu kuhusu hali zao katika maambukizi,”alisema.

Aliongeza kuwa kuna asilimia 38 katika ya watu 100 wanaoishi na virusi vya ukimwi hawajaweza kuwafikia.

Pia aliwataka  watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na wanajua hali zao wawe wanatumia dawa za ARVs.

“Kuna utafiti na ushahidi wa kisayansi unapotumia ARVs kwa kuzingatia masharti uwezo wa kuambukiza unapungua kwa zaidi  na asiyetumia ARVs ana nafasi ya kuambukiza watu wengi kuliko yule anayetumia,”alisema.

 Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji katika taasisi hiyo ya Benjamini William Mkapa, Dk. Ellen Senkoro alisema  wasanii ni kundi muhimu linaloweza kusaidia kufikia vijana kwa ukaribu.

Dk. Senkoro alisema taasisi hiyo inatambua vijana ni kundi mojawapo linalokabiliana na vishawishi vingi vinavyosababisha maambukizi ya ukimwi.

Alisema  semina hiyo wanawajengea uwezo wasanii kufikisha ujumbe jinsi inavyotakiwa kwa kuwa ni washawishi wazuri kwa lengo la  kuhakikisha wanapunguza kasi ya maambukizi , unyanyapaa na kuhimiza matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi.

Naye Mganga mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Yudas Ndungile alisema wizara ya afya  imejitahidi kuhakikisha inatoa elimu ya vvu kwa kupitia sanaa.

Naye Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Addo Novemba alisema, imekuwa ni desturi kwa wasanii kutangulizwa kufanya jambo hivyo wanaiomba wizara nyingine waige mfano huo kwa kuwa wanafanya kazi kubwa ya kuielimisha jamii.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho, William Chitanda alisema wasanii wapo tayari kushirikiana na wizara kuhakikisha sanaa zao zinapeleka ujumbe kwa wananchi na kuuelewa

Habari Kubwa