Mapigano kugombea malisho ya mifugo yasababisha vifo

15May 2022
Richard Makore
Tabora
Nipashe Jumapili
Mapigano kugombea malisho ya mifugo yasababisha vifo

​​​​​​​WATU watatu wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa wilayani Igunga mkoani Tabora katika mapigano ya kugombea maeneo ya  kulishia mifugo.

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao, alisema tukio hilo lilitokea juzi katika eneo la Isakamaliwa wilayani Igunga.

Alisema wananchi hao ambao walikuwa wanagombea maeneo ya kulishia mifugo, walitumia silaha za jadi kutekeleza mauaji hayo.

Kamanda Abwao alisema chanzo cha ugomvi huo ni kugombea sehemu ya kulishia mifugo yao na kwamba tayari msako wa kuwapata watuhumiwa wengine unaendelea baada ya watu wanne kukamatwa hadi jana kwa tuhuma za mauaji hayo.

Aliongeza kuwa matukio kama hayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu na kwamba ameagiza askari wake kuimarisha ulinzi wa usiku na mchana katika eneo hilo.

Kamanda Abwao alisema mtu mmoja aliyejeruhiwa katika tukio hilo anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga.

"Tumeweka ulinzi mkali katika eneo yalipotokea mauaji hayo na polisi watakuwapo saa 24 usiku na mchana ili kuhakikisha watu hawalipizi kisasi," alisema.

Kamanda huyo alisema mkakati wa kumaliza mgogoro huo uliogharimu maisha ya watu umeanza kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo.

"Lazima tuweke mipango endelevu ili kuhakikisha mauaji kama hayo hayatokei tena ili jamii iweze kuishi kwa amani muda wote," alisema.

Habari Kubwa