Mapinduzi yasherehekewa kivingine Z’bar

13Jan 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Mapinduzi yasherehekewa kivingine Z’bar

ZANZIBAR imeadhimisha kilele cha sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi kitofauti kwa kutumia muda mfupi bila
burudani za ngoma na halaiki.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), wakipita mbele ya jukwaa kuu katika maandamano ya sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar. PICHA: IKULU

Sherehe hizo zilianza saa moja na kumalizika saa tano asubuhi kwa maandamano na gwaride maalumu la vikosi vya ulinzi na usalama na baadae Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, kuhutubia wananchi. 

Sababu za kuchukua muda mfupi zilielezwa ni kutoa fursa kwa waumini wa dini ya Kiislamu kwenda kufanya ibada ya sala ya Ijumaa inayosaliwa saa sita mchana.

Licha ya sherehe hizo kuchukua muda mfupi, lakini zilifana na wananchi wengi walijitokeza katika Viwanja vya

Amani na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na marais wastaafu akiwamo Dk. Jakaya Kikwete,

Benjamin  Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, Dk. Amani Abeid Karume na Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilali.

Akihutubia katika sherehe hizo, Dk. Shein, alisema katika miaka 54 ya Mapinduzi, anajivunia kuimarika kwa huduma za elimu ambazo kabla, zilikuwa chache na zikitolewa kwa ubaguzi na kulipiwa.

Alisema hivi sasa shule za msingi zimeongezeka mara saba, za sekondari mara 53 na idadi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari imeongezeka mara 14 kutoka wanafunzi 25,372 mwaka 1963 hadi  378,211, mwaka 2017.

“Tatizo walilotutengenezea wakoloni kwamba watoto wa wafanyakazi na wakulima tusiingie sekondari na kupata elimu ya juu, leo halipo tena, haya ni mafanikio makubwa ya kuigwa,” alisema.

Alisema katika jitihada ya kuongeza madarasa, mwaka 2017 serikali ilianza ujenzi wa shule tisa za ghorofa za sekondari kwa Unguja na Pemba.

Alisema pamoja na hatua hizo, serikali inaendelea kushughulikia ununuzi wa madawati kwa ajili ya shule zote za Zanzibar ili kumaliza tatizo hilo.

Aidha, alisema kuanzia mwezi Julai mwaka huu, serikali yake itaanza kutekeleza azma ya kurudisha utaratibu wa kutoa elimu bure kwa shule zote za sekondari ili kutekeleza lengo la Mapinduzi.

“Kwa hivyo elimu ya msingi hadi sekondari itatolewa bure bila ya malipo,  kwa elimu ya msingi tayari ni bure,” alisema Dk. Shein.

Alisema pia serikali yake imepata mafanikio katika sekta ya afya kwa kuimarisha huduma za afya mjini na vijijini.

Alisema, kutokana na kuimarika kwa huduma hizo, vifo vya kinamama wanaojifungua vimepungua kutoka 237, mwaka 2016 hadi 195 mwaka 2017.

Alisema vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 54 mwaka 2010 hadi 43 mwaka 2017.

Hata hivyo alisisitiza kuwa maendeleo yanategemea amani na usalama wa nchi na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda nchi na kudumisha amani iliyopo.