Mapitio ya hukumu ya SP Bageni Juni 16

30May 2019
Hellen Mwango
DAR
Nipashe
Mapitio ya hukumu ya SP Bageni Juni 16

HATIMAYE Mahakama ya Rufani ya Tanzania imepanga kusikiliza mapitio ya hukumu ya kunyongwa ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni (kwa sasa mkoa wa kipolisi Kinondoni), Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni Juni 16, mwaka huu.

Maombi hayo ya mapitio yamefunguliwa mahakamani hapo na mshtakiwa yakiwa na sababu mbalimbali ikiwamo kupinga hukumu iliyotolewa Septemba 16, 2016.

Mapitio hayo yamepangwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Stella Mugasha, akisaidiana na Ferdinand Wambari na Rehema Kerefu.

Pamoja na mambo mengine, katika maombi yake, SP Bageni anapinga hukumu iliyotolewa katika mahakama hiyo chini ya jopo la majaji watatu likiongozwa na  Bernard Luanda akisaidiana na  Sauda Mjasiri na Senistocles Kaijage kwamba lilifanya makosa ya dhahiri.

Pia anadai kuwa jopo hilo lilifanya makosa katika mwonekano na kusababisha haki kutokuzingatiwa, hivyo kuomba mahakama itenguwe hukumu hiyo.

Septemba 16, 2016 mapema saa 3:45 asabuhi, msajili wa mahakama hiyo (kwa sasa Jaji wa Mahakama Kuu) John Kahyoza alisoma hukumu hiyo baada ya kusikilizwa kwa rufani iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

DPP alipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyowaachia huru aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na maofisa wenzake watatu akiwamo Bageni mwaka 2009.

Akisoma hukumu hiyo, Kahyoza aliwataja walalamikiwa kuwa ni ACP Zombe, SP Bageni, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Urafiki, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ahmed Makelle na Rajabu Bakari.

Alisema Mahakama ya Rufani ilipitia ushahidi uliotolewa Mahakama Kuu na kuona kwamba ilishindwa kuwatia hatiani washtakiwa wa mauaji na kwa kosa la kusaidia mauaji kufanyika.

"Kosa la kuua na kosa la kusaidia kuua ni makosa mawili tofauti, si sahihi kwa mtu aliyeshtakiwa kwa mauaji kutiwa hatiani kwa kosa lingine ambalo tangu mwanzo mshtakiwa alitakiwa kulijua ili kujitetea," alisema na kuongeza kuwa:

"Washtakiwa wote katika utetezi wao walipinga kuhusika katika mauaji hayo, lakini mlalamikiwa wanne, Rajabu alisema ukweli katika ushahidi wake kwa kueleza tukio la mauaji lilivyofanyika katika Msitu wa Pande, lakini ushahidi wake ulitakiwa kupokewa kwa makini na unatakiwa kuwapo na ushahidi mwingine wa kuunga mkono."

Akifafanua zaidi, Kahozya alisema: “Mlalamikiwa wa kwanza, Zombe, mahakama haikuona kama kuna ushahidi wa kumtia hatiani kwa mauaji wala kwa kusaidia kuua japo kuna jambo kichwani mwake analolifahamu kuhusu mauaji hayo. Ushahidi mwingine unaonyesha wajibu rufani watatu walishuhudia mauaji, lakini hawakuua."

Jopo, kwa mujibu wa Kahozya,  lilisema wamekubaliana kwamba watu wanne waliuawa kwa bunduki na mauaji yalikuwa ya kinyama katika Msitu wa Pande.

Mahakama hiyo ilijiuliza maswali kwamba je, wajibu rufani walikuwapo Pande? Jibu ni kwamba walalamikiwa wa pili, wa tatu na wa nne walikuwapo katika msitu huo na kwamba mlalamikiwa wa nne alisema ukweli mahakamani kuhusiana na tukio hilo.

Ilidaiwa kwamba mauaji hayo yalifanywa na askari Polisi Sadi, lakini mshtakiwa huyo hajawahi kushtakiwa. Mahakama inajiuliza waliouawa walipelekwa Pande kwa amri ya nani.

Kwa mujibu wa ushahidi, mahakama inajiuliza nini nia ya kuwapeleka watu hao Pande sehemu ambayo haina hata nyumba, mlalamikiwa wa pili, Bageni ndiye alitoa amri ya kuua, ushahidi unaonyesha washtakiwa waliwapeleka wakiwa hai Pande na waliwarejesha wakiwa marehemu.

"Marehemu walipelekwa huko ili tukio la mauaji lifanyike bila kipingamizi kwa kibali cha Bageni, ushahidi wa mlalamikiwa wa nne uliungwa mkono na tabia ya Bageni kwamba alikuwa akificha ukweli kuhusu mauaji hayo," alisema.

Hata hivyo, ushahidi wa maofisa watatu wa Jeshi la Polisi, wote walidanganya kwamba mauaji yalitokea Sinza katika majibizano kati ya Polisi na marehemu wakati wengine wa Sinza walisema hawakusikia tukio la aina hiyo kutokea.

"Mahakama hii imeona walalamikiwa wa kwanza, wa tatu na wa nne, rufani dhidi yao inatupwa hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani, mjibu rufani wa pili mahakama inatengua kuachiwa kwake kutiwa hatiani na Mahakama Kuu, inamuhukumu kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya watu wanne," alisema Msajili Kahyoza na kusababisha mahakama hiyo kulipuka kwa vilio.

Katika kesi ya msingi, Wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Morogoro waliouawa ni Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi, mkazi wa Manzese Dar es Salaam, Juma Ndugu.

Walidaiwa kutenda makosa hayo Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu wa Pande, uliopo wilayani Kinondoni baada ya kuwakamata wafanyabiashara hao Sinza, walipokuja Dar es Salaam kuuza madini.

Habari Kubwa