Mapokezi makubwa yamsubiri Mwinyi Z’bar

15Jul 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Mapokezi makubwa yamsubiri Mwinyi Z’bar

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, anatarajiwa kuwasili leo mjini hapa na kupokewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, asubuhi.

Baada ya kupokewa Dk. Mwinyi ataongozana na wafuasi wa CCM hadi Ofisi Kuu za CCM Kisiwandui na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Ali Mohamed Shein atamtambulisha rasmi mgombea huyo.

Atazuru kaburi la aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Mzee Abeid Amani Karume na baadaye kufanyiwa tambiko na wazee maalum wa CCM ili kupata baraka zao.

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alisema maandalizi ya mapokezi yameshakamilika na wanachama kutoka mikoa mitatu ya Unguja watampokea mgombea huyo.

Alisema Dk. Mwinyi atazungumza na wazee wa CCM kwa kazi ya kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar pamoja na kuitangaza ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Pia, atazungumza na wanachama katika uwanja wa makao makuu ya CCM Kisiwandui kwa mara ya kwanza baada ya uteuzi wake wa kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar.

“Hiyo ndiyo ratiba yetu fupi ya mapokezi ya mgombea wetu wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi...tumejipanga kumpatia mapokezi makubwa yenye shamra shamra mgombea wetu ambaye anakabiliwa na jukumu la kuhakikisha CCM inashika madaraka na kuongoza dola,” alisema.

Habari Kubwa