Mapya yaibuka askari wanaopambana ujangili

07Nov 2016
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Mapya yaibuka askari wanaopambana ujangili

WAKATI vita dhidi ya ujangili ikiwa imeimarishwa kwa kuunda kikosi maalumu na kuwekwa kwa Majenerali wawili kuongoza mapambano hayo, serikali imekiri kuwa askari wa ulinzi na usalama walioshiriki Operesheni Tokomeza mwaka 2013, wanaidai zaidi ya Sh. bilioni moja ambazo ni malipo ya posho.

Akizungumza na Nipashe katikati ya wiki iliyopita, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, alikiri kuwapo kwa deni hilo ambalo fedha za kujikimu.

Katibu Mkuu huyo alisema deni hilo linatokana na posho ya kujikimu kwa wiki mbili baada ya Bunge kusitisha operesheni hiyo na askari hao kutakiwa kubaki kwenye vituo wakisubiri maelekezo.

Awali, chanzo chetu kilisema askari hao wanadai posho ya Sh. bilioni moja, ikiwa ni malipo ya mwezi mmoja, hata hivyo.
“Hatujapokea malalamiko ya askari, lakini deni hilo lipo na linatambulika, tunalifanyia kazi. Ni kati ya madeni yaliyohakikiwa na yatalipwa," Jenerali Milanzi alisema.

Aidha, Jenerali Milanzi alisema deni hilo halitalipwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.

Taarifa za kuwapo kwa deni hilo zilikuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika Wizara ya Maliasili na Utalii kukagua meno ya tembo yaliyokamatwa na kikosi maalumu cha kupambana na ujangili.

WANA KINYONGO
Awali, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli aliieleza Nipashe kuwapo kwa deni hilo mapema wiki iliyopita, wakati akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kutokomeza ujangili nchini.

Lembeli alisema Rais anafanya kazi nzuri inayopaswa kuungwa mkono, lakini akadai wanaolinda mapori ya akiba na hifadhi za taifa bado wanakinyongo kutokana na kutolipwa stahiki zao zisizopungua Sh. bilioni moja.

Mbunge huyo wa zamani Kahama Mjini aliyekihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka jana na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema kuna uwezekano wa fedha hizo kutafunwa na wajanja wachache kiasi cha kutolipa stahili za watumishi hao na hadi sasa wanapigwa danadana.

“Hawa watu bado wapo porini, unafikiri wataifanya kazi kwa moyo mmoja?" Alihoji.

"Matumizi ya Sh. bilioni tatu zilizochangwa kwa ajili ya utekelezaji wa operesheni hii na Tanapa (Mamlaka ya Hifadhi za Taifa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na TFS (Wakala wa Misitu Tanzania) zilizoko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii hayajawekwa wazi hadi sasa.”

Lembeli alisema hadi Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, Balozi Khamis Kagasheki, anahojiwa na kamati yake kipindi hicho, alikuwa hajui kama fedha hizo zilikuwapo wizarani.

“Zilichangishwa, Kaghasheki hakujua kama zimechangishwa na zilichangwa kabla ya operesheni kuanza na zilivyopatikana zikawekwa kwenye mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori (Tanzania Wildlife Protection Fund (WPF) lakini hadi sasa matumizi yake hayajulikani na askari hawajalipwa stahili zao.

“Matatizo yamejitokeza (kulalamikiwa na kusitishwa kwa operesheni), Waziri anaulizwa na kamati fedha zilitoka wapi, zilikuwa wapi na nani alikuwa mtunzaji, hakuwa anajua. Kwa hiyo, matumizi ya fedha na kama kulikuwa na udanganyifu ulifanyika wizarani.

"Je, askari wanaodai fedha za operesheni hiyo na wapo porini hadi sasa, wataendelea kufanya kazi ya kupambana na ujangili kwa moyo mmoja?"

Kuhusu hofu hiyo ya Lembeli ya askari kupungua morali ya kazi, Jenerali Milanzi alisema: “Siamini askari aliyeajiriwa unasema utashindwa kupambana na ujangili, kama ni askari wa ujangili ni vyema kutofautisha ile ilikuwa ni operesheni lakini kuna askari ambao ‘is your day to day work’ (ni kazi yako ya kila siku) wanalipwa kwa ajili hiyo.”

Alisema kwa sasa wanahimiza uwajibikaji zaidi kwa kuwa pamoja na madai ya posho wanachotakiwa ni kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

"Kwa kuwa huwezi kuona majangili ukawacha kwa madai hujalipwa."

Meja Milanzi alisema kwa sasa kinachofanyika ni kazi ya kawaida kupambana na ujangili na siyo operesheni.

Kuhusu matumizi ya Sh. bilioni 3, alisema utaratibu wa fedha unajulikana na kwamba wanaolalamikia hawajui utaratibu.
“Utaratibu wa fedha ulifanyika, sikuwepo wakati huo lakini naamini hilo lilifanyika,” alisema Katibu Mkuu huyo.

Katika ripoti hiyo iliyosomwa bungeni Desemba 2013, Kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe tisa ilipewa jukumu kutathmini na kuangalia jinsi mpango wa Kupambana na Majangili ulivyopangwa na kutekelezwa na Serikali kupitia Operesheni Tokomeza.

Operesheni tokomeza ilianza Oktoba 4, 2013 na kusitishwa Novemba mosi, 2013 ambapo jumla ya kesi 687 za ujangili zilifunguliwa zikihusisha watuhumiwa 1,030.

Kwa mujibu wa Ripoti iliyowasilishwa Bungeni Desemba 2013, washiriki wa operesheni tokomeza walikuwa ni askari wanyamapori, usalama wa taifa, polisi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Lembeli alisisitiza vita dhidi ya ujangili nchini haitaisha kama madhambi yaliyoainishwa kwenye Ripoti ya Tokomeza hayatafanyiwa kazi, ikiwamo vigogo walioko serikalini waliotajwa kwenye ripoti kushughulikiwa.

“Magufuli ana kazi ngumu sana," alisema Lembeli. "Mtu huwezi kufanya biashara ya meno ya tembo bila kupata msaada au kinga ya vigogo wa Wizara au taasisi nyeti. Its simple (ni rahisi).”

Habari Kubwa