Marafiki wasimulia walivyomjua Gamba

20Oct 2018
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Marafiki wasimulia walivyomjua Gamba

WAKATI mwili wa mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW), Isaac Gamba, ukitarajiwa kusafirishwa kuja nchini kwa mazishi, marafiki zake wamesimulia wanavyomjua na walivyowasiliana naye siku za karibuni.

 Isaac Gamba enzi za uahi wake picha na mtandao

Gamba alikutwa juzi nyumbani kwake Ujerumani akiwa amefariki dunia baada ya kutoonekana ofisini kwa siku mbili ingawa chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika.

Mtoto wa dada yake mkubwa, Mayasa Maduga, ambaye ni askari Magereza, alisema msiba upo Mongo la Ndege jijini Dar es Salaam.

"Hatujapata taarifa kamili mwili utakuja lini lakini habari ambazo bado hazijathibitishwa na wenzetu wa Ujerumani, mwili unaweza kuwasili Jumapili (kesho) ya wiki hii," alisema.

Rafiki wa karibu wa Gamba, Aboubakar Liongo, aliandika jana kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa hadi sasa wameambiwa kuwa baada ya uchunguzi kukamilika ndipo mwili utasafirishwa kuletwa Tanzania.

Enzi za uhai wake, Gamba aliwahi kuwa mtangazaji wa Radio Free Africa, Radio Uhuru, ITV/Redio One na baadaye alihamia DW Ujerumani akiendeleza taaluma yake ya utangazaji hadi umauti unamkuta.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe, akizungumza na waandishi wa habari jana alieleza kushtushwa na kifo cha Gamba ambaye alikuwa rafiki yake mkubwa.

Mwambe alitoa kauli hiyo kabla ya kuanza kwa mkutano uliomhusisha yeye na Balozi wa Marekani nchini Tanzania.

Akielezea anavyomjua Gamba, mkurugenzi huyo alisema ni miongoni mwa marafiki zake wakubwa ambao hivi karibuni walikutana kwenye ndege wakiwa safarini kwenda Ujerumani.

Alisema walikaa karibu kwenye safari hiyo na walibadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo na kuhusu maendeleo yake alikokuwa akifanyia kazi.

 "Tulikutana kwenye ndege lakini kiti nilichokaa kilikuwa mbali na yeye, aliponiona alikuja kukaa kwenye kiti cha pembeni yangu. tulimwomba jirani yangu ambaye alikuwa nami ahamie kiti kingine na  alikubali ndipo mimi na Gamba tukakaa pamoja hadi Zurich, Uswisi," alisimulia.

"Tulizungumza mengi na tulipofika Zurich tuliachana pale yeye alikuwa anakwenda Bonn na mimi Beijing, China," alisema Mwambe.

Naye Liongo aliandika kwenye mitandao ya kijamii akielezea namna walivyokutana naye kikazi.

Liongo aliandika hivi kwenye ukurasa wake wa Facebook "Boss ili tukamate anga yote namhitaji kijana mmoja yuko Mwanza Radio Free Africa anaitwa Issac Gamba"

Liongo alisema ni maneno aliyomwambia aliyekuwa bosi wake Radio Uhuru, Mohamed Juneja, ambaye alikubali na kutaka atumiwe tiketi ya ndege ili afike Dar es Salaam haraka.

"Juneja akasema basi aje, ongea naye akikubali tumtumie tiketi ya ndege aje haraka sana, hiyo ni baada ya kumfuatilia hewani.

Gamba akawasili Dar es Salaam baada ya wiki moja akafikia kwa kaka yake Chang'ombe Polisi na siku hiyo hiyo nikamchukua hadi nyumbani kwangu, Ilala Sharrif Shamba,” Liongo anaeleza kuwa ilikuwa siku ya Jumamosi mwaka 2001.

"Mke wangu Alma alimpa chakula, nikamwambia usajili mpya kutoka Mwanza baadaye nikampa taulo akaoga akavaa nikampa koti langu jeusi tukaondoka watatu kwenda Njenje..kuanzia hapo tukaishi pamoja kazini na nje ya kazi.

 "Gamba au mwanangu kama tulivyokuwa tukiitana kweli umeondoka!! juzi tu hapa tulikuwa sote na hata siku moja kabla ya kuondoka tuka-enjoy na kuongea mengi sana pale Governors. Nilikuja Bonn mwaka jana nikawa nalala kwako na kwa Bundes (Kitojo). Weupe wa roho yako ukakujengea marafiki wengi pale Bonn," aliandika.

Aliongeza kuwa: "Nilijivunia kuwapo kwako pale. Umetutonesha kidonda cha Misanya Bingi, moyo wangu Gamba unabubujikwa na machozi ya damu.Kati ya nguzo zangu pale Bonn imeanguka nitauangalia vipi mji wa Bonn? Sitatamani tena kwenda Pendel ambayo ni pub palipokuwa kijiwe chako.

"Sitotamani tena kwenda Taccos Pub ambayo nilitambulisha akapapenda. Gamba tulipanga mengi sana kumbe Mungu alikuwa akipanga yake. Kwaheri Muyenjwa! kwaheri ya kuonana kijana wa kutoka Musoma uliyekuwa na roho ya upendo wa ajabu, kijana ambaye hukuthamini mali wala hela…nenda mwanangu wape salamu makomredi waliotangulia, iko siku tutaonana," anamalizia.