Marehemu amuuzia
kiwanja marehemu

16Jan 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Marehemu amuuzia
kiwanja marehemu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, imebaini rushwa ilihusika katika kutolewa kwa hati ya kiwanja kilichodaiwa kuuzwa na kutiwa saini na mtu ambaye tayari alishafariki dunia.

Katika taarifa ya utendaji wake kwa miezi mitatu iliyopita kuanzia Oktoba, mwaka jana, iliyotolewa jana na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, ilielezwa kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, walichunguza na kubaini kuwapo kwa rushwa katika sakata hilo.

“Tulifanya udhibiti ikiwa ni sehemu ya jukumu letu kwa mujibu wa Kifungu cha saba cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007. Moja kati ya mengi, ulihusu marehemu kumuuzia kiwanja marehemu,” alieleza Makunga katika taarifa hiyo.

Alifafanua kuwa uchunguzi wa Takukuru katika sakata hilo, ulibaini familia moja baada ya baba yao kufariki dunia, walimchagua mmoja wa wanafamilia ambaye pia alipitishwa na mahakama kusimamia mirathi ya marehemu baba yao.

Aliendelea kueleza kuwa wakati mwanafamilia huyo anaomba kuhamisha umiliki wa kiwanja cha marehemu baba yake kwenda kwenye umiliki wake, alianza kuzungushwa na mmoja wa maofisa ardhi na badaye alijulishwa na ofisa ardhi huyo kwamba marehemu baba yake tayari alishauza kiwanja hicho na umiliki ulishahamishiwa kwa mtu mwingine.

“Udanganyifu huu uliwezekana kufanyika kwa kuwa kuna vitendo vya rushwa vilifanyika,” alieleza Makunga katika taarifa hiyo.

Aliongeza: "Kwa kuwa msimamizi wa mirathi na watoto wote wa marehemu walikuwa na uhakika kwamba, katika enzi za uhai wa marehemu baba yao hakuwahi kuuza kiwanja na mali zilizoko kwenye kiwanja hicho, walileta malalamiko hayo kwetu.

"Baada ya uchunguzi wetu, tuliweza kubaini kwamba, marehemu hakuwahi kuuza kiwanja hicho bali kinachodaiwa kuwa ni mkataba wa mauziano ilikuwa ni nyaraka ya kughushi kuanzia tarehe ya mkataba, saini za marehemu pamoja na saini na muhuri wa kamishina wa viapo.

"Kwa msingi huo, Takukuru ilielekeza kwa watendaji wa mamlaka inayohusika, wabadilishe umiliki wa kiwanja hicho kwenda kwa msimamizi wa mirathi anayestahili na hivyo kufanikiwa kudhibiti vitendo vya rushwa katika eneo hilo na hatimaye haki kuonekana ikitendeka."

Habari Kubwa