Marekani yatoa bil. 5.6/- kusaidia afya TZ

23May 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Marekani yatoa bil. 5.6/- kusaidia afya TZ

SERIKALI ya Marekani imetangaza kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (Usaid), kuongeza Dola za Kimarekani milioni 2.4 (Sh. bilioni 5.6), ikiwa ni msaada kwa sekta ya afya Tanzania.

Msaada huo unalenga kuimarisha uwezo wa maabara na upimaji wa kimaabara, kusaidia jitihada za utoaji taarifa, miradi ya maji na usafi wa mazingira, kuzuia na kudhibiti maambukizo, kutoa elimu ya afya kwa umma na miradi mingine.

Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani jana, ilisema fedha hizo ni nyongeza ya msaada wa Dola za Kimarekani milioni moja, unaolenga kusaidia mapambano dhidi ya janga la Covid-19, uliotolewa hivi karibuni na kufanya kiasi kipya cha fedha zilizotolewa kwa Tanzania ili kukabiliana na janga hilo kufikia Dola milioni 3.4.

Kiasi kingine cha Dola milioni 1.9 zimebadilishwa matumizi na kuelekezwa kwenye mapambano dhidi ya janga hilo.

“Hii inafanya jumla ya fedha zote zilizotolewa na Marekani katika kukabiliana na Covid-19 nchini Tanzania hadi hivi sasa kufikia Dola za Kimarekani milioni 5.3 (Sh. bilioni 12.2),” ilisema taarifa hiyo.

“Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Marekani imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 7.5 kwa maendeleo ya Tanzania huku karibu Dola bilioni 4.9 zikielekezwa kwenye sekta ya afya pekee. Toka mwaka 2009, Serikali ya Marekani imetoa zaidi ya Dola bilioni 100 kusaidia miradi ya afya na takriban Dola bilioni 70 kama msaada wa kibinadamu duniani kote,” iliongeza taarifa hiyo.

Serikali ya Marekani inaendelea kuwa mfadhili mkubwa zaidi duniani wa miradi ya afya na shughuli za kibinadamu zinazolenga maendeleo ya muda mrefu na jitihada za washirika wake kujijengea uwezo na kuchukua hatua za dharura wakati wa majanga.

“Tunaongoza duniani katika utoaji wa misaada ya kibinadamu na kiafya katika kukabiliana na janga la Covid-19,” iliongeza taarifa hiyo.

Watu wa Marekani wametoa zaidi ya Dola bilioni 10 zitakazosaidia jitihada za kimataifa zakukabiliana na Covid-19. “Tutaendelea kuhakikisha kuwa mchango mkubwa wa kifedha na wa kisayansi wa Marekani katika mapambano haya unabaki kuwa kitovu na sehemu ya jitihada za pamoja na zilizoratibiwa vyema za jumuiya ya kimataifa dhidi ya Covid-19.

Ikiwa ni miezi kadhaa sasa tukipambana na janga hili nchini kwetu na nje ya nchi yetu, Marekani inaendelea kuongoza jitihada za kimataifa dhidi ya mlipuko huu, ikijenga katika uzoefu wa miongo kadhaa ya uongozi katika utoaji misaada ya kiafya inayookoa maisha na misaada ya kibinadamu.”

Habari Kubwa