Marekani yawamwagia wanawake bil. 1.1/-

21Mar 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Marekani yawamwagia wanawake bil. 1.1/-

SERIKALI ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa (Usaid), imetoa msaada wa Dola za Marekani 500,000 sawa na Sh. bilioni 1.1 kusaidia wanawake 500 watakaotaka kugombea uongozi.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk. Inmi Patterson, alisema hayo jana, wakati wa uzinduzi wa mradi wa awamu ya pili uliolenga kuwajengea uwezo wanawake kupata uongozi katika nyanja mbalimbali ikiwamo katika siasa.

Dk. Patterson alisema mchango huo unajumuisha mafunzo ya masuala ya kisiasa na michakato ya uchaguzi, kutimiza malengo ya muda na jinsi ya kumudu ratiba za chama na uteuzi.

Alisema serikali ya Marekani itachangia kulea na kutoa mafunzo kuhusu usimamizi wa kampeni, jinsi ya kuandaa ujumbe na kutumia sera.

Aidha, alisema katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, kaulimbiu ya ‘usawa bora’ inaendana na mazingira ya Tanzania kwa sasa wakati ikiongeza kasi ya maendeleo yake kuelekea uchumi wa kati.

“Nchi zisipotilia mkazo kujenga uwezo wa wasichana na wanawake zinasahau kwamba wanawake waliojengewa uwezo wana uwezo wa kuleta mageuzi kwenye jamii,” alisema.

Alisema ukosefu wa elimu na afya ni vikwazo ambavyo vinasababisha wasichana na wanawake washindwe kuishi maisha ya kujitosheleza na kuchangia kutokuwapo kwa usawa katika jamii.

Dk. Patterson alisema changamoto kubwa kwa  wanawake wengi ni kukosa nguvu, ushawishi na sauti ya kufanya uamuzi muhimu unaohusu maisha yao na kutenda kwa uhuru bila kuogopa.

Aidha, alisema wanawake wamekuwa na uwakilishi hafifu kwenye michakato ya kisiasa na uchaguzi na changamoto hiyo haiko kwa Tanzania pekee.

Balozi huyo alisema hali hiyo inaonyesha kwa kiasi kikubwa jinsi wanawake wanavyotengwa kwenye nafasi nyingi za juu za kufanya maamuzi kwenye serikali kuu na vyama vya siasa.

Dk. Patterson alisema kauli ya uwezeshaji wanawake imetumika zaidi duniani, hivyo kuna haja ya kuwepo kwa mabadiliko ya kweli ambayo yataleta usawa katika fursa na kuondoa mila zinazowaondolea thamani.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Masuala ya Wanawake, (UN Women) Hodan Addiu, alisema wanawasaidia wanawake kupata uongozi katika masuala ya siasa na kushiriki uchaguzi.

Alisema wameshirikiana na serikali ya Marekani katika kuwainua wanawake kupitia mradi huo wa awamu ya pili, washiriki kupata uongozi kwa kuwapatia mafunzo ambayo yatawajengea uwezo.

Naye Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Sophia Mwakagenda, alisema kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge alipatiwa mafunzo hayo ambayo yamemsaidia kujiamini na kuweza kuuliza maswali bungeni.

Aliwashauri wanawake wajitokeze kwa wingi ili wapatiwe mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kugombea nafasi za juu za uongozi wanapoelekea katika uchaguzi.

Habari Kubwa