Marufuku kutoa vibali upimaji ardhi kampuni binafsi

02Mar 2021
Rose Jacob
MWANZA
Nipashe
Marufuku kutoa vibali upimaji ardhi kampuni binafsi

SERIKALI imepiga marufuku halmashauri zinazotoa vibali vya upimaji ardhi kwa kampuni binafsi ili kupima maeneo ya wananchi badala yake kazi hiyo ifanywe na watumishi wa sekta ya ardhi.

Kauli hiyo ilitolewa leo mkoani Mwanza na Waziri  wa Ardhi, Nyumba na  Maendeleo na Makazi,  William Lukuvi wakati akitoa hati za kumiliki ardhi  kwa wananchi wa kata ya Kisese wilayani Magu.

Amesema kuanzia sasa ni marufuku mtendaji yeyote wa serikali katika sekta ya ardhi kuzipa kazi  kampuni za upimaji badala yake watumishi wafanye wenyewe  na kama hawatoshi wachukue wanafunzi wa Chuo cha Ardhi  mkoani Morogoro  ili kukamilisha kazi ya upimaji na uchoraji ili kupanga miji.

Aidha, Lukuvi amewataka watendaji wa wizara yake kuwasaidia wananchi kupata hati za kumiliki ardhi ili waweze kuzitumia kukopa benki.

"Hata ukiwa na nyumba nzuri, viwanja vingi hauwezi kukopesheka, lakini kinachokopesheka ni kuwa na hati miliki hiyo tu ndiyo inayoweza kuvunja milango ya benki na  kumuondolea umaskini mwananchi hivyo wapimieni na muwamilikishe  ardhi watu ili waondokane na presha ya viwanja," amesema Lukuvi.

Lukuvi ameagiza wilaya zote nchini zitambue maeneo yote ya vijiji vipya ili kuwaelekeza kujenga kwa mpangilio."Toeni elimu kwa wananchi kule ambako kuna sifa halmashauri isimamie wajenge kwa mpangilio, kijiji kikiwa na kiasi cha kuanzia Shilingi milioni nane kinaweza kupangiwa matumizi bora ya ardhi.Kamishina msaidizi  wa ardhi, Elia Kamiyanda alisema wamepokea kiasi cha Sh. milioni 220 kwa ajili ya upimaji wa viwanja 3,000 katika vitongoji vitatu vya Wita A,  Igudija na Kitumba vilivyopo kata ya Kisesa.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Magu,  Merchdes Wema, amesema viwanja 2,612 kati ya 3,000 vimeishatambuliwa na kuwekewa mawe ya upimaji vikiwamo  viwanja ya 34 kwa matumizi ya viwanda vikubwa na vidogo katika kitongoji cha Ihushi kata ya Bujashi.

Habari Kubwa