Marufuku mikusanyiko Mbeya

25Jul 2021
Nebart Msokwa
Kyela
Nipashe Jumapili
Marufuku mikusanyiko Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya amepiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote kufanyika ndani ya mkoa huo ili kuepuka kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona, akisisitiza kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayekiuka katazo hilo.

Juma Homera alitangaza katazo hilo jana wilayani Kyela alipozungumza na wananchi wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo.

Aliliagiza Jeshi la Polisi kutekeleza alichokiita kuwashughulikia watu wote watakaofanya mikusanyiko hiyo.

Homera alisema ugonjwa wa corona upo na unagharimu maisha ya watu, hivyo serikali haitakuwa na uvumilivu dhidi ya wanaohamasisha mikusanyiko, akidai wao wameshachanjwa na hawana hofu ya kupata maambukizi.

“Sisi tunazuia maambukizi, tunataka vifaa vya kuwasaidia madaktari kuwahudumia wananchi vizuri, lakini kuna watu wanataka mikusanyiko na mikusanyiko yoyote lazima iwe na kibali, sasa wewe jichanganye huko, tukikufurumisha usije ukalalamika,” alionya.

Aliliagiza Jeshi la Polisi kusimamia katazo hilo kwa kuhakikisha watu hawafanyi mikusanyiko katika eneo lolote ndani ya mkoa huo yakiwamo maandamano yanayohamasishwa na baadhi ya vyama vya siasa.

Vilevile, aliliagiza jeshi hilo kuhakikisha watu wote wanaopanda vyombo vya usafiri wa umma, wanavaa barakoa kabla ya kupanda vyombo hivyo na kuhakikisha vyombo hivyo zikiwamo daladala zinabeba abiria kulingana na uwezo wake ili kuepusha misongamano.

Homera pia aliwataka wananchi kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono ili kuepuka maambukizi ya virusi hivyo.

“Mkiangalia hapa mimi na DC (Mkuu wa Wilaya) na viongozi wengine ambao nimeambatana nao, tumevaa barakoa kwa ajili ya kujilinda na tatizo hili, hivyo ninawashauri nanyi mshone barakoa zenu na mzivae, siyo lazima ununuwe, wewe jishonee ya kwako,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Homera alisema ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, serikali imeongeza wasambazaji wa dawa kutoka mmoja mpaka wanne ili vituo vyote vya kutolea huduma za afya viwe vinapata dawa kwa wakati mkoani humo.

Aliwaagiza wakuu wa wilaya zote za mkoa huo kuunda kamati maalum za kukagua maduka yote ya watu binafsi wanaouza dawa za binadamu ili kubaini kama hakuna dawa za serikali zinazouzwa huko na watakaobainika kuuza dawa hizo, lazima wachukuliwe hatua za kisheria.

“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya watumishi wa afya, dawa za serikali zikiingia wanasema mgodi umetema, wanaiba dawa, wanakwenda kuziuza kwenye maduka ya watu binafsi.

"Sasa tutafanya upekuzi mpaka nyumbani kwa watumishi wa afya na tukizikuta lazima tutawajibishana," alihadharisha.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Agelina Lutambi, aliwataka wananchi wa mkoa huo kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (CHF) ili iwasaidie kupata huduma za matibabu kila wanapougua.

Alisema magonjwa huwa hayapigi hodi na wakati mwingine huwa yanakuja wakati ambao mtu anakuwa hana akiba yoyote na hivyo akasisitiza kuwa mfuko huo unasaidia wakati kama huo.

Habari Kubwa