Marufuku silaha katika mikusanyiko

21Jul 2021
Francis Godwin
IRINGA
Nipashe
Marufuku silaha katika mikusanyiko

WAZIRI  wa  Mambo ya  Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amepiga marufuku ya kuingia na silaha kwenye maeneo ya starehe kama baa, kumbi za muziki, harusi na mengine yenye mkusanyiko.

WAZIRI  wa  Mambo ya  Ndani ya Nchi, George Simbachawene.

Katika kuhakikisha angalizo hilo linazingatiwa, ameagiza ni lazima kuwapo  utaratibu wa wahusika na maeneo hayo  kufanya ukaguzi mlangoni kabla ya watu kuingia ndani ya maeneo hayo tajwa.

Simbachawene alitoa agizo hilo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilisha ziara yake ya  siku mbili mkoani Iringa.

Ziara hiyo ilijumuisha kutembelea maeneo mbalimbali kikiwamo kiwanda cha Hong Wel International kilichoko mjini Mafinga.

Alisema wizara inaona kuna jambo la kujifunza kupitia tukio la mauaji yaliyotokea kwenye baa mkoani Dar es Salaam.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, maeneo ya Sinza mkoani Dar es Salaam, kijana aliyetambulika kwa jina la Alex Koroso, alidaiwa kumuua kijana mwenzake kwa na bastola kisha kujiua.

Simbachawene alisema kuwa kutokana na tukio hilo wanaona suala la umilikishaji wa silaha na utunzaji wa silaha lina dosari kubwa katika maeneo mengi.

Alisema anayemilikishwa silaha ni lazima awe ni mtu mwenye akili timamu na siyo mtu mwenye pesa asiye na akili timamu.

Simbachawene alisema umejitokeza utaratibu usio mzuri kwamba mtu akishakuwa na pesa tu, pasipokuwapo tishio lolote la usalama wake, anakimbilia kununua silaha, tena pasipo kufuata utaratibu wowote wa umilikishaji wa silaha.

"Mtu anayepewa kibali cha umiliki wa silaha lazima awe na akili timamu na awe ni yule mwenye tishio la kiusalama na siyo mtu kuwa na pesa lazima kumiliki silaha.

"Kwa sasa imejitokeza tabia ya baadhi ya vijana kumiliki silaha kama fasheni  na wengi wao wamekuwa wakienda maeneo ya starehe wakitamba kwa kuonyesha silaha hizo wanazomiliki  hadharani kuwa 'mimi nina bastola hapa', jambo ambalo ni kinyume cha sheria inayozingatiwa katika umiliki wa  silaha," alionya.

Alisema kumiliki silaha siyo sifa ama ufahari bali heshima kwa wamiliki wa silaha ni kuheshimu matumizi na vibali vyake.

Alisema wapo baadhi ya watu wanamiliki silaha na hawajulikani kutokana na kupata silaha hizo kupitia kwa madalali.

Alisema wizara yake imeanza mchakato wa kutambua wamiliki wa silaha na tayari baadhi ya watu waliohusika na utoaji wa vibali vya silaha wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi na ripoti kamili ya mchakato wa umilikishaji wa silaha inaandaliwa.

Katika ziara yake hiyo, waziri huyo pia aliwataka wawekezaji wanaofanya shughuli zao katika Wilaya ya Mufindi, kuendelea kufanya shughuli zao kwa utulivu na kuacha kufanyiana visa na kupigana.

Habari Kubwa