Marufuku wagonjwa kuonyeshwa tamthiliya

15Jan 2019
Ibrahim Joseph
Dodoma
Nipashe
Marufuku wagonjwa kuonyeshwa tamthiliya

SERIKALI imepiga marufuku runinga zote za hospitali za serikali kuonyesha wagonjwa vipindi vya kawaida kama tamthiliya badala yake waonyeshe vyenye kutoa elimu ya afya.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alipokuwa akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, baada ya kufanya ziara hospitalini hapo.

“Tulishatoa ‘flash’ bure za vipindi vya kutoa elimu ya afya kwenye hospitali zote za serikali, sitaki kuona runinga hizo zinaendelea kuonyesha vipindi vya michezo na vinginevyo vya kawaida,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema serikali kupitia wizara hiyo iliandaa vipindi vya kutoa elimu ya afya ili kuwasaidia wananchi wanaofika kupata huduma katika hospitali hizo kujifunza elimu hiyo.

Alisema wameandaa vipindi vya kuelimisha kuhusu lishe na elimu ya kujikinga na magonjwa mbalimbali pamoja na namna ya tiba za baadhi ya magonjwa hayo.

Aidha, aliziagiza hospitali zote za rufani nchini kuhakikisha wanafunga mifumo ya ukusanyaji taarifa za kitabibu kila idara kwenye hospitali zao.

Dk. Ndugulile aliziagiza hospitali hizo kuhakikisha zinafunga mifumo ya ukusanyaji wa taarifa zote za hospitali za kitabibu kila idara.

“Tunahitaji kupata taarifa za kila mgonjwa, muda aliofika, aina za vipimo pamoja na daktari aliyemhudumia na ahakikishe anasaini na taarifa zote hizo zinatakiwa kupatikana na kwenye mfumo wa aina moja,” alisema Ndugulile.

Alisema uwapo wa taarifa hizo utasaidia kuondoa ukakasi kama mgonjwa aliyefika hapo atashindwa kuhudumiwa ipasavyo.

“Kama hakuna mfumo maalumu wa kujua nani amemhudumia mgonjwa na ikitokea amepoteza maisha kwa uzembe inakuwa vigumu kujua wa kumwajibisha,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema mwongozo wa wizara unataka kila mgonjwa akifika hospitali taarifa zake ziandikwe kila idara anayofika kwa usahihi, tarehe, muda aliopokelewa na wale wote waliomhudumia waandike majina yao na saini zao.

Dk. Ndugulile alisema hospitali zote zinatakiwa kuja na mfumo wa aina moja ya ukusanyaji mapato ili kuepusha upotevu wa mapato.

Aliwataka madaktari kuandika majina sahihi ya asili ya dawa za matibabu wanazowaandikia wagonjwa na waandike taarifa kwa kutumia nyaraka sahihi za hospitali badala ya kutumia makaratasi ya kawaida.

Aidha, alisema serikali inakusudia kuanzisha utaratibu wa cheo cha ukurugenzi wa hospitali za rufani baadala ya cheo cha waganga wafawidhi wa hospitali hizo.

“Bado serikali tupo kwenye kipindi cha kuwachunguza wahusika kabla ya kuwateua kushika wadhifa huo mpya, tunataka watu wachapakazi na wenye uwezo wa kazi,” alisema Dk. Ndugulile.

Mkuu wa Kitengo cha Meno na Meneja wa Kitengo cha Bima ya Afya, Dk. Athanase Masele, alimwomba Naibu Waziri kusaidia kuzuia watumishi wa Hospitali ya Rufani ya Dodoma kuhamishiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Ernest Ibenzi, alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya ongezeko kubwa la wagonjwa na wingi wa wagonjwa wa msamaha.

Habari Kubwa