Masauni aihakikishia UNHCR kuwalinda wakimbizi

08Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Masauni aihakikishia UNHCR kuwalinda wakimbizi

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR), Kanda ya Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu, Clementine Nkweta-Salami, na kumhakikishia ushirikiano zaidi kati ya wizara yake na shirika hilo.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwa Mhandisi Masauni, jijini Dodoma jana yalijadili masuala mbalimbali ikiwamo uimarishaji wa ushirikiano hasa katika kuhakikisha wakimbizi wanalindwa na kuhudumiwa ipasavyo.

Naibu Waziri Masauni alimhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa Tanzania itaendelea kulinda haki za wakimbizi kama ilivyokuwa ikifanya kwa miaka mingi, na pia inasimamia zoezi la kuwarejesha kwa hiari nchini kwao wakimbizi kutoka Burundi.

“Nikuhakikishie tu, Serikali ya Tanzania inawajali wakimbizi, ndio maana kwa miaka mingi inaendelea kuwahifadhi, hivyo katika kipindi hiki cha kuwarejesha nchini kwao tunahakikisha wanarudishwa wakimbizi wote kwa hiari,” alisema Masauni.

Alisema mazungumzo zaidi kuhusu wakimbizi waliopo nchini yatajadiliwa zaidi na kukubaliana katika mkutano wa pande tatu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Naibu Waziri alimshukuru Mkurugenzi huyo ambaye aliambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo hapa nchini, Chansa Kapaya.