Masele: Nimelelewa vyema

21May 2019
Sanula Athanas
Dodoma
Nipashe
Masele: Nimelelewa vyema

HATIMAYE Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele, amehojiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka kuhusu tuhuma za utovu wa nidhamu, huku akisisitiza amelelewa vyema na wazazi na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele (kushoto), akihojiwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Bunge, jijini Dodoma jana. PICHA: OFISI YA BUNGE

Hatua hiyo ya kuhojiwa kwa Masele imetokana na agizo la Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, kuandika barua kwa Rais wa PAP kumtaarifu kusitisha uwakilishi wa mbunge huyo na kumtaka kurejea nchini kuhojiwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Wakati Spika Ndugai akitangaza uamuzi huo Jumatano, Masele ambaye pia ni Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), alikuwa Afrika Kusini akishiriki vikao vya PAP.

Huku Spika Ndugai akilieleza Bunge kuwa Masele amekaidi mara kadhaa kurejea nchini kuhojiwa, jana saa 3:40 asubuhi, mbunge huyo aliingia bungeni na baadaye saa 5:34 asubuhi aliingia kwenye chumba cha mahojiano na Kamati ya Maadili iliyomhoji hadi saa 9:18 alasiri.

Kabla ya kuhojiwa na kamati hiyo, Masele ambaye mwaka 2010 alitangazwa kushinda kiti cha ubunge kwa tofauti ya kura moja, aliingia kwenye ukumbi wa Bunge kisha akaingia kwenye maktaba ya Bunge na baadaye kuingia kwenye mgahawa wa chombo hicho cha kutunga sheria.

Saa 5:10 asubuhi, Masele alitoka kwenye mgahawa huo na kufanya mazungumzo ya dakika nne na Mbunge wa Bariadi Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali, Andrew Chenge.

KAULI YA MASELEBaada ya kuhojiwa na Kamati ya Maadili, Masele aliwaambia waandishi wa habari kuwa ameitikia wito wa Bunge, huku akisisitiza hajawahi kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu katika kipindi chote akiwa kiongozi.

Alisema amelelewa vyema na wazazi wake na CCM aliyoitumikia katika ngazi mbalimbali kuanzia akiwa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) hadi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.

"Mimi nimelelewa vizuri na wazazi wangu na chama kuanzia ngazi ya chini hadi juu, nimekuwa kiongozi UVCCM, mjumbe wa baraza kuu la chama, natambua miiko ya kiuongozi na sijawahi kufanya kosa la utovu wa nidhamu," alisema.

Masele aliongeza: "Nilichofanya ni kutetea misingi ya haki za binadamu. Isitafsiriwe kwamba ni utovu wa nidhamu."

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka, baada ya kumhoji Masele, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanaendelea kufanya uchambuzi wa shauri lake na wakimaliza kazi, watakabidhi taarifa kwa Spika.

Habari Kubwa