Mashahidi 19 kuitwa kesi ya bangi

23May 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mashahidi 19 kuitwa kesi ya bangi

UPANDE wa Jamhuri umepanga kuita mashahidi 19 katika kesi ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi kilo 128.54 inayomkabili Gudluck Mbowe na Ally Mtema.

Madai hayo yalitolewa jana na Jamhuri katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa maarufu kama ya Mafisadi, iliyoketi chini ya Jaji Immacula Banzi.

Wakili wa Serikali Costantine Kakula, alidai kuwa mbali na mashahidi 19, pia watawasilisha na vielelezo mbalimbali ikiwamo mabegi saba ya bangi na gari moja aina ya Toyota IST.

Akiwasomea maelezo ya awali, Kakula alidai kuwa washitakiwa hao walikamatwa Oktoba 15, mwaka 2017 eneo la Kibaha kwa Matiasi baada ya polisi kupewa taarifa kwamba watu hao wamebeba dawa hizo za kulevya.

Ilidaiwa kwamba, washitakiwa walibeba mabegi saba ya bangi katika gari lao aina ya Toyota IST.

Pia, ilidaiwa kuwa siku ya tukio, polisi eneo la Kibamba walijaribu kusimamisha gari hilo, lakini hawakusimama na dereva aliendelea kuendesha kwa mwendo kasi.

Polisi walikimbiza gari hilo hadi lilipoingia mtaroni na kupata ajali na washitakiwa walikamatwa na upekuzi ulipofanyika.

Upekuzi huo ulihusisha washitakiwa pamoja na shahidi wa kujitegemea na kufanikiwa kukamatwa kwa mabegi saba ya bangi.

Hati ya upekuzi ilijazwa na kusainiwa na washitakiwa pamoja na shahidi huyo. Katika mahojiano washitakiwa hao walikiri kubeba dawa hizo za kuevya.

Ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilithibitisha kwamba mzigo huo ni dawa za kulevya aina ya bangi kilo 128.54.

Habari Kubwa