Mashine feki EFD zazagaa kila kona

21Mar 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Mashine feki EFD zazagaa kila kona

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema imebaini kuzagaa kwa mashine feki za EFD ambazo zinatumiwa kutoa risiti feki maeneo mbalimbali nchini hali ambayo inaikosesha serikali mapato.

Aidha, imesema wapo wafanyabiashara wanaotoa risiti za viwango vidogo tofauti vya kiasi halisi ili kukwepa kodi, jambo ambalo ni uhujumu uchumi.
 
Hayo yalisemwa jana na Kamishana Mkuu wa TRA, Charles Kichere, wakati akifungua mkutano wa washauri wa kodi Dar es Salaam pamoja na mtoa mada ambaye pia Ofisa Msaidizi wa Kodi wa Mamlaka hiyo, Honest Njau.
 
Mkutano huo uliofunguliwa na Kichere, ulijadili changamoto na uboreshaji katika masuala ya ukusanyaji wa kodi ili kuinua ulipaji wa kodi kwa hiari.
 
Akiwasilisha mada kuhusu mashine za EFD, Njau alisema ziko mashine feki (ghost machines) ambazo hutumika kutoa risiti feki na kuikosesha serikali mapato.
 
Njau alisema wanazitambua mashine hizo kutokana na aina ya risiti zinazotolewa kuwa na maandishi yenye ukubwa tofauti na zile sahihi na kwamba hatua zinachukuliwa kila wanapobainika.
 
Akifungua mkutano huo, Kichere alisema wafanyabiashara wengi wanapofanya mrejesho wa kodi, ndipo katika ukaguzi TRA inabaini risiti feki za EFD, jambo ambalo linaonyesha kuna vishoka wa kutengeneza risiti hizo.
 
"Mfanyabiashara anaeleta madai ya kodi ya mabilioni ya fedha lakini ukifuatilia kwa kina unakuta fedha anayodai ni ndogo na zilizobakia ni risiti feki," alibainisha na kuongeza:
 
"Mtu analeta madai ambayo hayapo, anataka kuchukua kiasi cha fedha tulichokusanya, hii ni sawa na wizi, anaiibia serikali. Lakini ukifuatilia washauri wa kodi wamezipitisha kuwa ni madai halali, ndiyo maana tunasema kwa sasa tutawaripoti kwenye vyombo vyao vya kitaaluma," alibainisha.
 
Aidha, alisema TRA imebaini kuwa mashine za EFD hazifanyi kazi inavyotakiwa kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanadanganya kwa kutoa risiti zisizo sahihi.
 
"Tumebaini wako baadhi ya wafanyabiashara wanafanya mauzo ya Sh. 800,000, lakini wanatoa risiti ya Sh. 500,000 au chini ya hapo, lengo ni kukwepa kodi. Hii si sahihi kabisa na wanahujumu uchumi," alisema Kichere.
 
Alisema jambo hilo halikubaliki kwa kuwa mashine hizo zimetolewa kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara lakini wanazitumia kuhujumu, ili TRA isipate kodi yoyote na kwamba uchunguzi unaendelea ikiwamo kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola wanaofanya mtindo huo.
 
Aidha, alisema wako washauri wa kodi ambao wanaleta marejesho ambayo hayako sahihi na kwamba TRA imeshawabaini na hatua za kisheria zitachukuliwa baada ya kufikishwa kwenye kamati.
 
Kamishna huyo alisema baadhi ya wahasibu wa wafanyabiashara nchini wanahujumu uchumi kwa kutengeneza vitabu na hesabu feki ili kukwepa kulipa kodi.
 
Kichere alisema wahasibu hao huwa na vitabu vya kupeleka benki, TRA na halmashauri vyote vikiwa na mahesabu tofauti.
 
 "Katika ukaguzi wetu tulimkuta mhasibu mmoja ana vitabu vitano ambavyo vyote kwa mwaka mmoja vina hesabu tofauti. Cha mauzo ya Sh. bilioni 142, kingine Sh. bilioni 80 na kinachokuja TRA Sh. bilioni 18," alisema na kuongeza:
 
"Kuna wahasibu sita tumewaripoti kwenye Bodi ya Wahasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) kama chombo chao cha kitaaluma ili wachukue hatua," alisema.
 

Habari Kubwa