Mashirika 8 ndege za nje kuanza safari nchini

26May 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mashirika 8 ndege za nje kuanza safari nchini

MASHIRIKA manane ya ndege yametangaza kurejesha safari zao za ndege za kuingia na kutoka mipaka ya Tanzania kuanzia Jumatatu ijayo.

Baadhi ya mashirika hayo yametangaza ndege zake kuanza safari zake Julai mosi kwa kutua Dar es Salaam, KIA, mkoani Kilimanjaro na Zanzibar.

Kwa mujibu wa tovuti ya Rick shaw travel group, inayojishughulisha na usafirishaji watalii kwenda kwenye vivutio mbalimbali kwa takribani miaka 32, safari hizo zitakuwa kwa nchi za Afrika Mashariki na kuishia kwenye viwanja vya ndege nchini.

Juni mosi, Shirika la Ndege la Tanzania linatarajia kurejesha safari zake za kuelekea Entebbe, nchini Uganda na siku inayofuata itakwenda Hahaya, Harare na Lusaka nchini Zambia.

Juni 3, safari zitakuwa Dar es Salaam kuelekea Mumbai, nchini India na Julai 2, itaelekea Bunjumbura, nchini Burundi.
Kwa upande wa Shirika la Ndege la Emirates linatarajia kuanzia Julai 2, kutokea Dubai.

Shirika la Ndege la Ethiopian Airlines, kutoka Addis Ababa, litaanza tena Juni mosi safari za ndege za kila siku kwenda Dar es Salaam, KIA na Zanzibar.

Nalo Shirika la Ndege la Kenya Airways lina mpango wa kuanza tena kutoa huduma zake nchini Tanzania kuanzia Julai 10 na zitatua katika viwanja vya ndege vya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Zanzibar.

Shirika la Ndege la KLM, linatarajia kuanza safari zake Julai 4, kutoka Amsterdam kuelekea Kilimanjaro, Dar es Salaam.

“Shirika la Ndege la Qatar Airways lina mpango wa kuwa na ruti moja kwa siku ya usafiri kuanzia Julai 15, kati ya Dar es Salaam na Doha. Usafiri wa kuelekea Kilimanjaro hautakuwapo hadi Agosti 31, kilisema chanzo hicho.

Shirika la Ndege la Swiss litaanza safari zake kuanzia Julai mosi kupitia Nairobi kwenda Dar es Salaam na ndege hizo zitakuwa zikitokea Zurich.

Kwa upande wa Turkish Airlines, litarudisha safari zake zote za usafiri wa ndege kama kawaida kuanzia Juni 28 kama hali itakuwa nzuri.

Mashirika mengine ya ndege, Rwanda, Afrika Kusini na mengineyo hadi sasa hayajatoa taarifa zao na wengi wameonyesha kuahirisha hadi Mei 31.

Habari Kubwa