Masogange yamkuta ya Wema Sepetu kortini

03Aug 2017
Hellen Mwango
Dar es salaam
Nipashe
Masogange yamkuta ya Wema Sepetu kortini

MKEMIA Elias Mulima (40), amedai mahakamani kwamba alipokea sampuli ya mkojo wa msanii Agnes Gerald Waya maarufu Deal ama Masogange (28) na alipoufanyia vipimo alipata majibu kuwa anatumia dawa za kulevya aina ya heroin na oxazepam.

Masogange.

Mulima ambaye pia ni Meneja wa maabara ya Mkemia Mkuu na shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alidai kuwa alibaini chembechembe hizo baada ya kupima sampuli ya mkojo wa mshtakiwa.

Ushahidi huo ulisikilizwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Juzi katika kesi inayomkabili Wema Sepetu na wenzake, Mulima aliiambia mahakama hiyo vipimo vya mkojo wa mshtakiwa huyo vilionyesha ni mtumiaji wa bangi.

Shahidi huyo alitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba juzi.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Costanine Kakula jana, shahidi huyo alidai kuwa Februari 15, mwaka huu akiwa ofisini kwake, askari wawili wa Jeshi la Polisi walifika ofisini kwake wakiwa na mshtakiwa Masogange.

Alidai kuwa alipokea maelekezo na kuchukua sampuli ya mkojo wa Masogange na kuufanyia vipimo ili kubaini kama anatumia dawa za kulevya au la.

"Nilimpa mshtakiwa kontena maalumu kwa ajili ya kutolea sampuli hiyo... niliuchanganya na kemikali zinazochukua dawa za kulevya kwenye mkojo na nilipima kwenye mitambo maalumu," alidai shahidi.

Akifafanua zaidi, Mulima alidai kuwa baada ya uchunguzi alibaini kwenye mkojo huo kuna chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroin na oxazepam.

"Mtumiaji wa ulevi wa dawa za kulevya sio salama, hautibiki kirahisi na inasababisha ugonjwa wa akili," alidai mkemia Mulima.

Alidai kuwa baada ya majibu kutoka aliandaa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na sampuli ya mkojo huo na ilithibitishwa na Kaimu Mkemia Mkuu.

Alidai kuwa anamtambua mshtakiwa kuwa ndiye aliyepima sampuli ya mkojo wake siku ya tukio, na akaiomba mahakama kupokea taarifa ya uchunguzi huo kama kielelezo.

Hata hivyo, wakili wa utetezi Nehemia Nkoko alipinga taarifa hiyo kupokelewa kwa maelezo kwamba ina upungufu wa kisheria.

Upande wa Jamhuri uliomba pingamizi hilo litupwe kwa sababu halina mashiko na kwamba mshtakiwa alikiri mahakamani kuchukuliwa na kupimwa sampuli ya mkojo wake kwa Mkemia Mkuu.

Hakimu Mashauri alisema Agosti 28, mwaka huu atatoa uamuzi wa shauri hilo kama taarifa hiyo ipokelewe au la.

MKOJO WAKE
Juni 13, mwaka huu mshtakiwa Masogange aliposomewa maelezo ya awali dhidi yake katika kesi hiyo alikiri kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kutoa sampuli ya mkojo wake na kupimwa.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana shtaka la kutumia dawa hizo.

Katika kesi ya msingi, Masogange anakabiliwa na mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin na oxazepam.

Pia, 'supa staa' huyo anadaiwa kufanya makosa hayo chini ya kifungu cha 18 (a) cha Sharia ya Kupambana na Dawa za Kulevya, namba 5 ya mwaka 2015.

Katika kesi hiyo namba 77 ya mwaka 2017, Masogange anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya heroin (Diacety Imophine).

Pia anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya oxazepam.

Masogange yupo nje kwa dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja alisaini bondi ya Sh. milioni 10 na masharti kwamba mshtakiwa asitoke nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.

Habari Kubwa