Masoko yanavyokosa mabilioni- 2

17May 2018
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Masoko yanavyokosa mabilioni- 2

KATIKA toleo la jana tuliona jinsi mapato yanavyopotea katika masoko ya Manispaa za Jiji la Dar es Salaam kutokana na miundombinu duni, licha ya masoko kuwa chanzo kikuu cha mapato lakini jitihada za kujenga na kuboresha ili kukusanya fedha zaidi ni ndogo.

Kadhalika, Meneja biashara wa Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni, walieleza kiasi kinachokusanywa na iwapo miundombinu itaboreshwa kitakusanywa kiasi gani. Endelea...

Meneja wa masoko wa Manispaa ya Temeke, Johnson Makalanga, anasema kuna jumla ya masoko 25 kati yake 20 yanakusanya ushuru, lakini kuna changamoto kubwa ya miundombinu bora na makusanyo yanayopatikana ni kidogo.

“Soko la Temeke Sterio ndiyo kubwa lenye wafanyabiashara zaidi ya 4,000 na linaongoza kimapato. Linakusanya Sh. milioni 100 hadi 140 kwa mwezi na linalouza bidhaa zote za kutoka shamba ikiwa ni jumla na reja reja,” anasema.

Anasema soko jingine ni la Tazara linalokusanya Sh. milioni 14 kwa mwezi, likifuatiwa, Charambe  Sh. milioni kumi , Tandika Sh. milioni saba, na Mbagala Sh. milioni saba kwa mwezi.

Kwa mujibu wa Makaranga, kwa sasa masoko ya Manispaa hiyo yanaingiza Sh.bilioni 1.1, na kwamba ikiwa sheria ndogo mpya za mwaka 2017 zitapitishwa na Waziri kwa ushuru wa Sh. 300 kwa kila kizimba kwa siku, watakusanya Sh. bilioni 2.6 kwa mwaka.

Anasema kiasi hiki ni kidogo na hata ushuru ukipitishwa wa Sh. 500 kwa kila mfanyabiashara mwenye kizimba mapato yatafikia Sh. bilioni 2.6 na kingeweza kupatikana mara mbili ya kiasi hicho iwapo masoko yatakuwa na miundombinu mzuri.

KUPATA FEDHA

Diwani wa kata ya Kunduchi, Michael Urio, anasema kwa ujumla mapato mengi ya kwenye masoko yanapotea kutokana na miundombinu hafifu iliyopo na tungeweza kuyaboresha na kupata fedha na wakati huo huo kutoa huduma nzuri kwa kujiajiri na wanaofuata huduma.

“Mapato makubwa kwenye masoko yanapotea kwa kuwa huwezi kutoza fedha nyingi kwenye eneo ambalo hujaweka vizimba au viosk, tungeboresha tungekusanya fedha nyingi na kutoa huduma bora kwa wananchi wetu,” anafafanua.

Diwani huyo anaeleza mipango iliyopo ni kujenga masoko ya Tegeta Nyuki na kuboresha barabara ya kuingia na kutoka kwa bajeti ya Sh. bilioni 3 ili kukusanya fedha zaidi na wakati huo huo kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Tunatambua masoko ni chanzo muhimu cha mapato na tunajitahidi kuyaboresha kwa kadri bajeti inavyoruhusu. Siridhishwi na hali iliyopo kwenye masoko mengi, hakuna mpangilio na miundombinu ni duni,” anafafanua.

ASILIMIA 85 

Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Equality for Growth, Jane Magigita, anasema asilimia 85 ya Watanzania wako sekta isiyo rasmi na masoko ni chanzo kikubwa cha mapato na ajira, lakini hakuna anaeyajali zaidi ya kukusanya mapato tu.

“Tumefanya utafiti kwenye masoko ya Dar es Salaam na tumebaini mengi yamejaa, hayana mifumo ya maji taka, chemba zinamwaga majitaka ovyo, mabanda ni chakavu na hakuna vizimba vya biashara, sakafu, mpangilio mbovu, lakini cha kusikitisha kinachoangaliwa ni ukusanyaji wa fedha bila kuboresha chanzo husika,” anasema.

Anafafanua kuwa licha ya kuwa masoko ni chanzo cha ajira na mapato, lakini kutokana na kutoyaimarisha mapato mengi yanapotea na kinachokusanywa ni sawa na tone la maji kwenye bahari.

“Haya masoko yangeboreshwa vizuri yangekuwa ni sehemu ya utalii kwa wageni kutoka magharibi Jiji likapata fedha na hapo hapo Manispaa ikapata ushuru, lakini yameachwa kwa sababu ambazo hakuna anayeweza kuzieleza,” anasema.

Magigita anasema toka mwaka 2009 waanze kazi, kila Manispaa ilisema itajenga masoko ya kisasa, lakini hadi sasa hayajajengwa na cha kusikitisha, michoro iliyobuniwa siyo rafiki kwa biashara husika na hivyo upo uwezekano mkubwa wa kutofanikiwa.

Anasema mfano mzuri ni jengo la Machinga Complex ambalo lilijengwa kwa muundo wa ghorofa, lakini wafanyabiashara hawakunufaika nalo kwa kuwa wateja wako maeneo ya chini na hivyo kujikuta wanarudi eneo la chini.

“Watendaji wamebeba kauli za kisiasa wanakusanya fedha, lakini hawarudishi huduma kwenye masoko na kinachosemwa ni kuwa makusanyo ni madogo, hii yote ni kukosa vipaumbele kwa fedha yote kuwekwa kwenye kapu moja na kufanya shughuli nyingine na kuacha kutumika kuboresha chanzo husika,” anafafanua.

"Huwezi kukamua ng’ombe bila kumpa malisho, masoko ya Dar ni mabaya sana, machafu, hayana mpangilio maalum na halmashauri zinashindwa kuyajali na kukamua maziwa (fedha) kila uchao bila kujali afya za watumiaji na walaji." UWEZEKANO KUKOPA 

Wakati Manispaa za Dar es Salaam zikilia ukata wa kukosa fedha za kuboresha masoko, kuna Mfuko wa Bodi ya Mikopo wa Serikali za Mitaa, unaotoa mikopo kwa ajili ya kuboresha chanzo cha mapato ya halmashauri.

Zipo halmashauri nchini zilizotumia mfuko huo zikajenga masoko ya kisasa.

Lakini pia, Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa (Local Government Loans Board), inatoa mikopo kwa halmashauri kwa ajili ya kuboresha vyanzo vya mapato, huku suala hilo likiruhusiwa na sheria ya fedha kwa halmashauri kukopa.

Katika tovuti ya LGLB, masharti ya mikopo ni kutoa mchango wa akiba, kuandaa andiko la mradi na kuwasilisha kwenye Bodi, mradi upitishwe na baraza la madiwani, uwe mahususi wenye manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa halmashauri na kuchangia asilimia 20 ya gharama ya mradi husika.

Mengine ni mkopo urejeshwe kwa kipindi cha muda maalum kulingana na ukubwa wa mradi kwa riba ya asilimia 13 kwa mwaka, marejesho ya mkopo yatatokana na vyanzo vya mapato vya halmashauri na iwapo watashindwa kurejesha kwa wakati watapigwa faini ya asilimia moja, halmashauri iwasilishe taarifa iliyothibitishwa na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kuonyesha jinsi suala la mazingira litakavyosimamiwa.

Miradi inayopewa kipaumbele na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ni ujenzi wa masoko na minada, vituo vya mabasi, kumbi za mikutano, majengo ya utawala, uzalishaji wa umeme, miradi ya shamba la miti, uvuvi na uboreshaji wa barabara.

Tangu kuanza kwa Bodi hiyo jumla ya miradi 11 kutoka halmashauri na manispaa imetekelezwa ambayo ni ujenzi wa soko la Kiusa-Moshi, jengo la utawala Lushoto,vituo vya mabasi vya Musoma, Mbinga, Nyegezi Mwanza, Kishapu, jengo la utawala Igunga, upanuzi wa kituo kikuu cha mabasi Moshi Mjini, Hostel na ukumbi wa Benjamin Mkapa Mbeya na josho la ng’ombe Ushirombo, Bukombe. KUFUNGA MASOKO  

 Mwanasheria wa Baraza La usimamizi wa Mazingira (NEMC), Heche Suguta anasema Sheria inaruhusu Nemc kufunga masoko ambayo hayakidhi vigezo vilivyotajwa kisheria kama wanashindwa kuwa na miundombinu ya kutiririsha majitaka, kuwa na majisafi na kuwa na vyoo vya kisasa.

Aidha, alisema kuwa wameshawahi kuchukua hatua kwa kufunga soko la Buguruni katika eneo la machinjio ya kuku ambayo yalikuwa hayakidhi viwango na kwamba mengi hayana miundombinu inayokidhi vigezo.

Nipashe ilitembelea masoko ya Kiusa na Soko Kuu Manispaa ya Moshi, pamoja na Mwanjelwa Mbeya, na kuona jinsi walivyojenga miundombinu bora, ambayo imeongeza makusanyo na kukiwa na mikakati ya kuboresha mengine zaidi.

Masoko ya Kiusa na Soko Kuu, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro na Mwanjelwa, lililoko jiji la Mbeya, ni mifano halisi inayodhihirisha kwamba iwapo masoko yataboreshwa, yanaweza kuingiza mapato makubwa.

Soko la Kiusa ambalo kwa sasa limejengwa kisasa, linaingiza Sh milioni 38.5 kwa mwaka, huku awali lilikuwa linaingiza chini ya Sh. milioni 10 tu.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bernadetta Kinabo, kisheria Halmashauri inatakiwa kujenga soko au kuboresha chanzo cha mapato na kuwa na miundombinu bora ili kiweze kuingiza mapato zaidi, huku akieleza uzoefu unaonyesha kuwa halmashauri nyingi hazitoi kipaumbele kwenye uboreshaji wa vyanzo hivyo.

Anasema hakuna maelekezo ya moja kwa moja kwa halmashauri kuwa soko liwe na kiwango gani, bali hutegemea nguvu ya kichumi ya halmashauri husika, ikiwa ni pamoja na kipaumbele, uamuzi na elimu kwa wakurugenzi wa halmashauri husika.

Kwa mujibu wa Kinabo, wafanyabiashara wana haki ya kujengewa masoko ya kisasa ili wafanye biashara katika mazingira mazuri na inapotokea halmshauri haijafanya hivyo, wafanyabiashara wanaweza kuwa na makubaliano maalum ya kuboresha au kujenga soko.

“Kwa mfano, wakati tunapanga kujenga soko la Kiusa, tuliwasiliana na ofisa mipango miji, injinia na mimi (Mkurugenzi) waliamua aina ya soko watakalojenga,” anafafanua.

Anasema kabla serikali kuu haijachukua chanzo kikubwa cha mapato cha halmashauri, ambacho ni majengo kwa upande wa mijini na ushuru wa mazao kwa halmashauri za vijijini, kilikuwa ni nguzo ya mapato kwa halmashauri.“Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanakusanya kodi ya majengo na hivyo chanzo kimeondoka.

Katika maboresho ya halmashauri walikubaliana wakusanye na inarejeshwa kama ruzuku ya kuendesha halmashauri na ni chanzo kikubwa cha mapato kwa maana ya ruzuku, katika majukumu ya halmashauri moja wapo ni kutekeleza sera,” anafafanua.

Kinabo anasema soko la Kiusa lilijengwa kwa awamu baada ya sekretarieti kupeleka mapendekezo na kupitishwa na baraza la madiwani na kuridhia kuchukua mkopo uliosaidia kujenga hadi kumalizika.

“Wengi wanajiuliza niliwezaje kuthubutu kujenga masoko, siri ni kutokana na elimu ya kujenga masoko, semina na mafunzo, kutokana na juhudi za mtu (Mkurugenzi) katika kutekeleza majukumu, hali ya masoko,” anasema.

“Haikwepeki kuwa masoko ni chanzo kikuu cha mapato cha halmashauri, na ni jukumu lao kuyatengeneza, lakini wengi wa wakurugenzi bado hawajajua nini cha kufanya ili masoko yawe kipaumbele na kutengewa fedha au kutafuta mikopo,” anasema.

Anasema ili soko lijengwe ni lazima liwe ni kipaumbele cha halmashauri husika, lipitishwe kwenye bajeti kuanzia kwenye kamati na baadaye kikao cha bajeti cha baraza la madiwani.

Ofisa Habari wa Manispaa ya Moshi, Ramadhani Hamisi, anasema Manispaa hiyo kwa kutambua umuhimu wa masoko, ilijenga soko kuu kwa kutumia mapato ya ndani ambalo kabla ya maboresho lilikusanya Sh. milioni 30 na sasa linakusanya Sh. milioni 43.2 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko iliyokusanywa kabla ya maboresho.

Akieleza jinsi alivyofikia uamuzi wa kujenga soko la kisasa la Kiusa, Kinabo, anasema katika kufikiri nini cha kufanya ili kupata mapato mengi kwenye masoko, waliona kuna fursa ya kupata fedha na kuboresha masoko.

Anasema baada ya kubaini (sheria ya serikali za mitaa inaruhusu kukopa kwa ajili ya kuboresha chanzo cha mapato, hivyo alishirikisha baraza la madiwani wazo hilo ambao waliridhia na wakaamua wachukue mkopo kwenye Bodi ya mikopo kwa serikali za mitaa.

Ujenzi wa soko la Kiusa uligharimu Sh. bilioni moja, na lilijengwa kwa awamu kuanzia mwaka 2006 hadi 2009.Anasema halmashauri zinapata mapato makubwa kutokana na masoko kwa kuwa shughuli za ununuzi, usafirishaji na uuzaji zote zinaingiza pesa.

Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya, anasema mkopo wa soko hilo ulikuwa ni Sh. milioni 900 na zimelipwa zote hadi mwaka jana, na sasa wako kwenye mpango wa uboreshaji na ujenzi wa masoko mengine.

“Soko la Kiusa wakati linajengwa lilikuwa na wafanyabiashara 1,600 ikiwa ni vibanda, mabucha ambao walilipa kodi ya pango na wachuuzi ambao wanalipa Sh 200 kila siku,” anafafanua.

Kwa mujibu wa Mboya ambaye pia ni diwani wa kata ya Longuo, wako kwenye mpango wa kujenga soko kuu na kituo kikuu cha mabasi kwa kushirikiana na sekta binafsi baada ya kutangaza kuwa ni eneo la uwekezaji.

Anasema wamepata kibali cha kutangaza soko la Mbuyuni na kituo kikuu cha kimataifa mabasi cha Ngangamfumuni kitakachojengwa kwa fedha za serikali Sh. bilioni saba, Moshi kuwa ni eneo la uwekezaji ili kupata wawekezaji wa kujenga na hivyo Moshi kuwa na masoko ya kisasa yatakayowawezesha kuongeza wigo wa kupata fedha kutokana na chanzo hicho.

Kauli ya umuhimu wa kujenga masoko ya Kinabo, inaungwa mkono na Meya huyo anayesema chanzo cha mapato kinapokuwa ni kipaumbele cha halmashauri kitaboreshwa na kufanywa kuwa cha kisasa zaidi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato.

“Moshi tumeona masoko ni chanzo kikubwa cha mapato ndiyo maana toka siku nyingi tumechukua mkopo kwa ajili ya kuboresha na tunaendelea kuyaboresha yote,” anasema na kuongeza:

“Tunachofanya kabla ya kutafuta wawekezaji tunaboresha yaliyopo ili wafanyabiashara wawe katika hali nzuri, masoko mengi bado yako kama gulio, likiboreshwa linarahisisha ukusanyaji wa mapato.” SOKO KIMATAIFA

Kama ilivyo kwa soko la Kiusa, Manispaa ya Moshi, Jiji la Mbeya liliamua kuboresha soko la kimataifa la Mwanjelwa, kwa kukopa Sh. bilioni 13 benki ya CRDB na kujenga soko la kisasa.

Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilingi, anasema soko hilo ni la kimataifa na lina uwezo wa kupokea wafanyabiashara wa kila aina kwa kuwa limejengwa kukidhi matakwa ya wote huku Jiji jilo likipata fedha.

Meneja wa soko la Mwanjelwa, Upendo Mungano, anasema kila mwezi wanatakiwa kuilipa benki ya CRDB Sh. milioni 40 na kwamba mapato ni kati ya Sh. milioni 70 na kuna miezi inafika hadi mil 400 iwapo mabenki na wapangaji wa taasisi watalipa kodi kila baada ya miezi mitatu.

“Baada ya ujenzi wa soko kodi ilikuwa Sh. 550,000 kwa eneo la chini kwa mwezi na juu Sh. 250,000, lakini tulifanya mabadiliko mwaka jana na kuwa Sh. 200,000., Sh. 50,000 na 15,000. Tulipunguza bei ili kupata wajeta wengi na kuwazoesha wafanyabiashara soko,” anasema na kuongeza:

“Mapato ya soko yanatakiwa kuwa Sh. milioni 100 wa mwezi iwapo kila eneo litakuwa limepangishwa, tuna maeneo ya mabenki, vizimba, maduka na kuna maeneo ya maduka ya ‘super market’ na migahawa.”

Anasema soko lina vizimba 456 kati yake 179 ndiyo vinawapangaji, eneo la meza lina watu 120 kati yake 78 ndivyo vimepangishwa, kwenye ghorofa ya kwanza kuna maduka 102 kati yake 85 yana wapangaji, huku ghorofa ya pili kukiwa na vibanda 88 kati yake 12 vinawateja, na maeneo ya wazi wakiwa 78 kati yake 48 yana wateja, vibanda vya machinga vipo 343 vyote vimepangishwa na maeneo ya mabenki.

Meya huyo anafafanua zaidi kuwa soko limekuwa na miundombinu bora, matarajio ni kutengeneza faida na hivyo kuweza kurejesha mkopo husika kwa wakati.

Akizungumzia changamoto, Meya huyo, anasema soko hilo lilijengwa kwa muundo wa ghorofa, na wateja wengi hawapendi na hivyo ukusanyaji wa mapato bado si mzuri kama ilivyotarajiwa. MCHUMI UDSM

Mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Razack Lokina, anasema masoko katika nchi nyingi duniani ni chanzo kikubwa cha mapato iwapo yataboreshwa na kuwa na miundombinu bora.

“Masoko yanatakiwa yatoe ajira na serikali ikusanye kodi ambayo itatumika kuimarisha miundombinu kwenye masoko,” anasema.

Kwa mujibu wa Profesa huyo, kama miundombinu ni mibovu ni dhahiri kuwa mapato hayatapatikana kama inavyotarajiwa na hivyo kuathiri uwezo wa serikali wa kuhudumia miundombinu iliyopo.

“Ni lazima miundombinu iimarishwe na mapato yakusanywe na taratibu nzuri ziwepo za kuyasimamia. Haitarajiwi serikali itoe ruzuku kwa ajili ya kuendesha masoko bali masoko ndiyo yanatakiwa yatoe mchango kwenye uchumi wa nchi kwa upana wake,” anafafanua. SHERIA YA FEDHA

Sheria ya fedha ya serikali za mitaa sura 290 inaruhusu halmashauri kutoza kodi, ushuru kwenye masoko na ada mbalimbali kutoka kwenye vyanzo mbalimbali watakavyovianzisha kupitia sheria ndogondogo kutokana na vyanzo vya mapato vilivyopo.

Sheria hizo zinatoa majukumu manne kwa halmashauri. Kusimamia uchumi pamoja na maendeleo ya kijamii katika halmashauri, na hapa ndipo masoko yanapoingia kama chanzo cha mapato.

Pia, sheria inasisitiza ubora wa vyanzo vya mapato kama masoko kuwa na miundombinu bora kwa kuhakikisha shughuli za kiuchumi na maendeleo ya kijamii, afya, mazingira, barabara na elimu zinakuwa katika hali nzuri. MAZINGIRA SAFI

Mwezine Hussein aliyefanya biashara kwenye soko la Kiusa kwa zaidi ya miaka 20, anasema miundombinu ya sasa ni ya kuridhisha ambayo inawawezesha kuwa kwenye mazingira safi tofauti na awali hakukuwa na mpangilio mzuri, hakuna sakafu, vizimba na miundombinu ya majitaka na majisafi.

“Kwa sasa mfumo wa majisafi na majitaka uko vizuri, kipindi cha mvua hatupati bughudha ya bidhaa zetu kuharibika, tuna vizimba vya kisasa, uondoshaji wa taka unafanyika kwa wakati, hatunyeshewi na mvua, wateja wanakuja kwenye vibanda vya biashara” anasema.

Mmoja wa wanunuzi, Martha Fatael, alisema kwa ujumla miundombinu ya soko Kuu na Kiusa inaridhisha na siyo bugudha kwa watumiaji, huku akiiomba Manispaa kuweka mipango wa kuboresha masoko mengine kama ya Mbuyuniili serikali iendelee kupata fedha.

Habari Kubwa