Matapeli watumia jina la Jenerali Mboma

31Jan 2016
Nipashe Jumapili
Matapeli watumia jina la Jenerali Mboma

Matapeli wa mtandaoni wameingilia barua pepe ya Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Robert Mboma na kuomba msaada wa Dola za Marekani 2,550 kwa watu zaidi ya 1,000.

ROBART MBOMA (KULIA) AKISALIMIANA NA MAKAMU WA RAIS MSTAAFU DK. GHARIB BILAL

Watu hao ambao bado hawajafahamika waliingia barua pepe ya Mboma Alhamisi na kutuma ujumbe kwa watu 1001, wakiwamo watu mashuhuri, wakiomba msaada huo.

Akizungumza na Nipashe Jumapili, Jenerali Mboma alisema katika tukio hilo ambalo limemshtua, watu hao baada ya kuingilia barua pepe hiyo walianza kutuma maombi ya msaada kwa watu ambao wapo katika barua pepe ambayo amekuwa akiitumia kwa mawasiliano na watu wake.

Alisema katika ujumbe huo ambao umeandikwa kwa lugha ya kiingereza, matapeli hao wameeleza kuwa Mboma amekwama katika mji wa Odesa, nchini Ukraine ambako alikwenda kwa mapumziko akiwa na familia yake.

Katika ujumbe huo ambao Nipashe imeuona, matapeli hao wameeleza kuwa Mboma akiwa nchini Ukraine alipatwa na tukio la kuibiwa pesa, pasi za kusafiria, simu na kadi za benki katika hoteli aliyofikia.

Walieleza kuwa Mboma baada ya kupata mkasa huo alikwenda kutoa taarifa polisi na ubalozini ambao walifanya jitihada kubwa katika kushughulikia tatizo hilo.

Matapeli hao walizidi kueleza kuwa, hata hivyo, Mboma na familia yake wameshindwa kurejea nchini kwa sababu amezuwiliwa na uongozi wa hoteli aliyofikia hadi alipe deni la Dola 2,550 ambazo ni gharama za siku alizokaa hotelini hapo.

Kufuatia hali hiyo, Jenerali Mboma aliwaomba watu wote waliotumiwa ujumbe huo kuupuuza kwani ni mchezo uliofanywa na matapeli kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia haramu.

“Mimi nipo Mbezi jijini Dar es Salaam, sijasafiri kwenda nchi yeyote kwa muda sasa, mliotumiwa ‘email’ msithubutu kutuma hizo pesa," alisema na kueleza kuwa "hao ni matapeli na uchunguzi utafanyika kuwanasa.”

Utapeli wa aina hii umeibuka kwa kasi nchini ambapo kwa mara ya mwisho matapeli walitumia jina la Waziri wa Sheria na Katiba, Dk.Harrison Mwakyembe kuomba msaada kwa watu mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara.

Habari Kubwa