Matatani tuhuma mauaji ya mpenzi

24Mar 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Matatani tuhuma mauaji ya mpenzi

JESHI la Polisi mkoani Mbeya, linamshikilia kijana aliyetajwa kwa jina la Festo Maduhu mwenye umri kati ya miaka 28 mpaka 30, mkazi wa Kabwe jijini Mbeya kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, picha mtandao

Maduhu anatuhumiwa kufanya kitendo hicho wakiwa kwenye nyumba ya kulala wageni.

Aidha, kijana huyo anatuhumiwa kujaribu kujiua kwa kujichinja koromeo baada ya kumuua mpenzi wake akikwepa kukamatwa na Polisi wakati akifuatiliwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alisema tukio hilo lilitokea Machi 22, mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi ambapo kijana huyo alimuua mpenzi wake, Jesca Michael (28).

Kamanda Matei alisema kijana huyo alimuua mpenzi wake huyo kwa kumkaba shingo na kumshushia makonde sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo usoni wakiwa ndani ya moja ya chumba cha kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Negero, ambayo mwanamke huyo alikuwa anafanyia kazi kama mhudumu.

Alisema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kwa maelezo kuwa maelezo kuwa Maduhu alikuwa anamtuhumu mpenzi wake huyo kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamme mwingine, ambaye jina lake limehifadhiwa.

“Mtuhumiwa alikutwa amejifungia nyumbani kwake na baada ya askari kuvunja mlango wa nyumba hiyo, alikutwa anaendelea kujichinja koromeo na askari walimwokoa na kumpeleka katika Hospitali ya Kanda ya Rufani ya Mbeya kwa ajili ya matibabu,” alisema Kamanda Matei.

Kamanda Matei alisema mwili wa Jesca umehifadhiwa katika hospitali hiyo, na mtuhumiwa anaendele kutibiwa akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.

Alisema baada ya kupatiwa matibabu hayo na kupata nafuu atahojiwa na Polisi kisha atafikishwa mahakamani.

Habari Kubwa