Matatani tuhuma za kutaka kumtapeli DC

11Jul 2019
Mary Geofrey
Nipashe
Matatani tuhuma za kutaka kumtapeli DC

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dar es Salaam, inamshikilia Omary Chuma (55), mkazi wa Chamazi wilayani Temeke, kwa tuhuma za kujifanya Ofisa Usalama wa Taifa Ikulu,-

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.

-kwa lengo la kutaka kumtapeli Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Takukuru, Ally Mfuru, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 2, mwaka huu, baada ya Takukuru kupokea taarifa ya kutaka kumtepeli mkuu huyo wa wilaya.

Alisema mtuhumiwa huyo alitenda makosa yaliyo chini ya sheria ya namba 11 ya mwaka 2007 kwa kosa la kujifanya Ofisa wa Serikali kinyume cha kifungu namba 100 (b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyorekebishwa mwaka 2002.

Alisema kosa lingine ni kuomba au kushawishi au kujaribu kujipatia au kujipatia rushwa kinyume cha kifungu 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Mfuru alisema ni wiki tatu zimepita tangu Takukuru itangaze kukamata watu sita wakiwamo wanne waliojifanya maofisa wa Takukuru na maofisa wa vyombo vingine na dola na wawili kutoka kampuni za simu.

Alisema matapeli hao wana mtandao unaojusisha maofisa mbalimbali wa Serikali ambao wanafuatilia watumishi au viongozi ambao kwa namna moja nyingine wanaweza kuwa na tuhuma, hivyo kuwadai fedha au rushwa huku wakijidai wao ni maofisa wa Takukuru au Usalama wa Taifa.

“Kwa mara nyingine tena tunatoa wito kwa matapeli wanaofanya vitendo hivi kuacha mara moja kwa sababu Takukuru ipo macho na ina mamlaka kisheria kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika na utapeli,” alisema.

“Mtuhumiwa huyu alitenda makosa hayo katika wilaya ya Kisarawe atafikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya hiyo leo (jana) Julai 10 kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabili,” alisema

Habari Kubwa