Mateso ya kuishi na mashine yamlazimu kuomba msaada

19Jul 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Mateso ya kuishi na mashine yamlazimu kuomba msaada

HAMAD Awadhi (28), anaishi kwa mateso ya kulazimika kutumia mashine ya kumsaidia kupumua (oxygen) muda wote hali inayomfanya aombe msaada kwa wafadhili wa kumwezesha kulipia gharama za umeme na gesi ya mashine hiyo ili aendelee kuishi.

HAMAD Awadhi.

Awadhi alikuwa amelazwa kwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Mloganzila na wiki iliyopita aliruhusiwa kutoka baada ya kukaa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Hospitali hiyo ilimsaidia mashine hiyo ya kupumulia yenye thamani ya Sh. milioni 3.5 ili kuokoa uhai wake na afya yake kuendelea kuimarika.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe jana nyumbani kwake Ukonga Majumba Sita, jijini Dar es Salaam, Awadhi anasema licha ya kupatiwa msaada huo, lakini anaishi maisha magumu.

Anasema angesaidiwa kupatiwa matibabu ya ugonjwa wake akapona ingemsaidia kuendesha familia yake kama ilivyokuwa awali.

Kwa sasa anasema kula yake ni ya shida na nyumba anayoishi ni ya kupanga ambayo anatakiwa kulipa kodi anayodaiwa.

“Kama unavyoniona hali yangu ni kuzunguka na hii mashine maishani mwangu, ningepatiwa msaada hata wa matibabu au wakaniwezesha kiuchumi ili niweze kuilea familia yangu maana kulala mwaka mzima hospitali kumenirudisha nyuma,” alisema.

 

UGONJWA ULIVYOANZA

Anasema Machi mwaka jana, alianza kuumwa kwa kuishiwa nguvu na kushindwa kupumua.

Alikwenda Hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam na kuanzishiwa matibabu na baada ya muda alipelekwa Hospitali ya Mloganzila.

“Nilivyofikishwa hapo Mloganzila niliwekwa katika chumba maalum kwa kuwa hali yangu ilikuwa ni mbaya kila wakati inabadilika, pumzi inakata na nguvu inaniishia,” anasimulia.

Alifanyiwa vipimo mbalimbali na jopo la madktari bingwa na majibu ya vipimo vilionyesha moyo wake umehama kutoka kushoto kwenda kulia na mapafu yamesinyaa hayana uwezo wa kupumua yenyewe.

“Ndio kama hivi siwezi kupumua bila mashine wakaniambia unahitaji kifaa cha kupumua maana uwezo wa kupumua bila mashine hauna,” anasema.

Alipatiwa barua ya kuomba msaada, lakini kutokana na hali yake alishindwa kuipeleka kwa watu kuomba msaada na kuendelea kukaa hospitalini hapo.

Ulipokuja uongozi mpya wa hospitali hiyo aliwasilisha maombi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dk. Julieth Magandi, ili aweze kupatiwa msaada.

“Viongozi wa hospitali hiyo walisikia kilio changu na kunipatia msaada wa hii mashine na kuruhusiwa kwenda nyumbani bila hivyo ungekuta nipo hospitali bila kujua hatima yangu ya kutoka.”

Pamoja na kupatiwa msaada wa mashine hiyo pia alifutiwa deni lake la zaidi ya Sh. milioni tisa ambazo asingeweza kuzilipa kutokana na kukosa uwezo wa kifedha.

"Viongozi wa hospitali yule mama Museru na wafanyakazi wote wamenipambania, bila Mloganzila nisingekuwa hapa wamenisaidia sana kwani hiyo hela nisingeweza kuilipa nina washukuru sana kwa msaada mlionipatia."

Alikuwa anaumia kuona wagonjwa wenzake wanaondoka na wengine kufa huku yeye akiendelea kuongeza siku hospitali.

“Mimi ni miongoni mwa wagonjwa waliokaa muda mrefu hospitalini hapo najulikana hospitalini hapo hadi getini kwa walinzi, yaani kama nilikuwa nipo nyumbani maana wafanyakazi wa hospitali lazima ukutane nao kila siku.”

AMWOMBA RC PAUL MAKONDA

Anasema changamoto kubwa baada ya kurejea nyumbani ni familia kumtegemea akiwa baba wa watoto wawili kwa kuwa mke wake hafanyi kazi.

“Ningeomba Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, anipatie hata msaada niweze kufungua biashara ambayo itaniwezesha kupata hela ya kuendesha familia yangu hata wasanii ama kampuni naomba mnisaidie napitia wakati mgumu,” aliomba.

Awali ililazimika kuuza baadhi ya vitu vya ndani ili kulipia matibabu yake na baadaye alishindwa kufanya hivyo ndipo hospitali ikamsamehe deni hilo.

Awadhi anasema kwa sasa anatakiwa kulipa kodi ya nyumba na gharama za umeme amepandishiwa kutokana na mashine hiyo kutumia umeme kila siku.

“Hii mashine inatumia umeme, ukikatika haifanyi kazi inanigharimu umeme na nyumba niliyopanga ina  wapangaji wengi inakuwa changamoto katika utumiaji wa umeme inanilazimu kuongeza fedha maana ninaonekana natumia umeme mwingi  kutokana na mashine hiyo kuwaka wakati wote.”

Anasema umeme unapokatika inamlazimu kutumia mtungi wa gesi ambao huwa anatakiwa kuujaza kwa Sh. 25,000.

“Mashine isipofanyakazi hapa utanionea huruma hali yangu inakuwa ni mbaya zaidi sasa ikatokea nikakosa hela ya kulipia umeme au huu mtungi wa gesi, uhai wangu unaondoka haya ni maisha magumu usiombe ukakutana na hili tatizo langu.”

Anasema wakati mwingi huwa anatumia dawa za kupuliza ambazo huzitumia kwa dakika chache anapotaka kwenda chooni kujisaidia ambazo huuzwa kati ya Sh. 18,000 na 25,000.

“Wakati mwingine nikiishiwa dawa hizo inanibidi nijisaidie ndani kwa vile siwezi kutoka na mashine hadi choo cha nje.”

Awadhi ambaye awali alikuwa anajishughulisha na ushushaji wa mizigo katika makontena Kariakoo, anasema kwa sasa anatafuta mtu amuuzie vifaa vyake vya nyumbani kwa kuwa maisha kwake yamekuwa ni magumu.

NDUGU WAMSUSA

Amesema baadhi ya ndugu zake hawana mawasiliano naye.

“Ndugu zangu wengine hali zao ni ngumu hao wengine kama wamenitenga fulani, maana mawasiliano tu ni shida nashukuru upande wa mama yangu na mke wangu unahangaika japo hali zao kiuchumi sio nzuri.”

Catherine Kurikana, mke wa Awadhi anasema hana biashara anayofanya kwa sababu alikuwa anamuuguza mumewe kwa muda mrefu.

Nyumba waliyokuwa wanaishia awali walihama kwa sababu ya kukosa kodi na kumlazimu kuhamia maeneo ambayo wapo ndugu zake ili wamsaidie.

Anasema familia yake ndio inahangaika kuwasaidia kwa chakula ingawa wakati mwingine wanapata mitihani ya kukipata.

“Hapa changamoto kubwa ni gharama ya kodi ambayo kwa mwezi ni Sh. 80,000 pamoja na umeme, kama ningekuwa na mtaji ningeanzisha biashara ili niendeshe familia maana mwenzangu ndio kama hivi ni mgonjwa kila kitu ananitegemea mimi.”

Habari Kubwa