Matetemeko yaendelea kutikisa Kagera

13Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Matetemeko yaendelea kutikisa Kagera

SIKU mbili baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Kagera lililosababisha vifo vya watu 16 Jumamosi, tetemeko jingine dogo limetokea katika mkoa huo, ingawa halikuwa na madhara.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salum Kijuu.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salum Kijuu jana aliliambia gazeti hili kuwa tetemeko dogo hilo lilitokea juzi saa 4:16.

Alisema tetemeko hilo lilidumu kwa sekunde chache.

“Ni kweli jana usiku kulitokea tetemeko lingine hata mimi nililisikia, lakini halikuwa kubwa sana, lilikuwa dogo na lilidumu kwa sukunde chache, ni watu wachache sana walilisikia,” alisema Meja Jenerali Kijuu.

Kuhusu tetemeko la Jumamosi ambalo lilikuwa na ukubwa wa 5.9 katika vipimo vya majanga hayo, Jenerali Kijuu alisema vifo vilivyoripotiwa kutoka hospitali ya mkoa wa Kagera vimebaki 16 na majeruhi ni 253.

Alisema kamati ya maafa ya Mkoa kwa kushirikiana na ile ya Ofisi ya Waziri Mkuu zinapita katika maeneo yaliyopatwa na tetemeko hilo ili kubaini athari iliyotokea pamoja na kufanya tathmini.

Juzi Mtaalamu mwandamizi wa Taasisi ya Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Gabriel Mbogoni aliliambia gazeti hili kuwa wananchi hao watarajie matetemeko madogo kuendelea kutokea.

“Tetemeko linaweza kuendelea kwa mwezi mmoja ama wiki mbili zaidi, mara nyingi huwa haiishi mara moja, lazima wananchi wajipange kwa hilo,” alisema.

Alisema pia kwamba tetemeko lililotokea juzi siyo la kwanza kwenye ukanda huo kwa kuwa kwa muda yamekuwa yakitokea mengine ndani ya ziwa Victoria.

Anasema tetemeko la sasa limeleta madhara zaidi kwa sababu limetokea nchi kavu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mtandao wa kompyuta wa earthquaketrack.com tetemeko hilo ndilo kubwa zaidi katika historia kutokea nchini.

Mbogoni alisema ni vigumu kubashiri ni lini matetemeko hayo yatatokea kwa sababu inahitajika utaalamu wa juu ambao nchini haupo.

Alisema hata baadhi ya nchi zilizoendelea ikiwamo Japan, wamekuwa wakishindwa kubashiri ni lini tetemeko litatokea.

Tetemeko hilo lilitokea alasiri ya Jumamosi, pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 zikipata nyufa, yakiwamo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Kufuatia tukio hilo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Kamati ya Maafa ambayo ipo katika Ofisi ya Waziri ya Mkuu itakwenda wilaya za Kyerwa, Karagwe na Bukoba mjini kwa ajili ya kufanya tathmini na kubaini athari zilizosababishwa na tetemeko hilo na kuona namna ya kuwasaidia waathirika.

Pia aliwaagiza viongozi wa mkoa huo kuchukua hatua za haraka kwa kuwatafutia eneo salama la kulala wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakato ambayo mabweni yake yote yameathirika na tetemeko hilo na hayafai kutumika.

Habari Kubwa