Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani inayoadhimishwa leo, Mrindoko alisema jana kuwa ndani ya matukio hayo, kuna matukio 887 yanayohusu ukatili dhidi ya watoto.
Mrindoko alisema visa vinavyoongoza katika takwimu hizo ni ubakaji, ulawiti, kutelekeza familia, ajira za watoto, vipigo na mimba za utotoni.
"Niombe sana familia kutenga muda wa kukaa pamoja kujadili mambo ya kifamilia, kufanya uamuzi na mipango ya pamoja. Hii inajenga upendo na mshikamano ikiwa ni pamoja na kufahamu maendeleo ya watoto nyumbani hadi shuleni na kuwapeleka sehemu za ibada ili kujenga jamii imara," alisema.
Mrindoko alizitaka familia zote kutimiza wajibu wao katika malezi ili kuondokana na wimbi la familia zinazotelekezwa pamoja na watoto wa mitaani.
"Familia ikipata mahitaji muhimu ya chakula, malazi, mavazi, ulinzi na upendo, ninaamini kabisa mambo haya ya ukatili hayawezi kutokea," alisema.
Mkuu wa Mkoa alisema vitendo vingi vya ukatili dhidi ya watoto vinafanywa na wanafamilia wenyewe, hivyo akaitaka jamii kuhakikisha inachukua hatua kuhakikisha mambo hayo yanakomeshwa.