Matukio ubakaji watoto yashika kasi

17Jun 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Matukio ubakaji watoto yashika kasi

CHAMA cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), kimeungana na taasisi nyingine kusherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika, huku takwimu zikionyesha matukio ya ubakaji yanashika kasi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben.

Aidha, Tamwa imeiomba serikali na wadau wengine wa masuala ya haki za watoto waendelee kupaza sauti zao ili kuhakikisha ukatili huu unapungua na ikiwezekana unamalizika kabisa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben, matukio ya ubakaji wa watoto ni tishio kwa usalama wao, ukuaji wao kwa ujumla na maendeleo endelevu ya taifa.

Alisema takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa mwaka 2018 watoto 2,365 walibakwa, idadi ambayo ni sawa na watoto 394 kwa siku.

Aidha, alisema ripoti ya hali ya uhalifu kwa mwaka 2017 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2017, matukio ya uhalifu dhidi ya watoto yalikuwa 13,457.

Pia kwa mwaka 2016 matukio hayo yalikuwa 10,551, na kwamba kati ya hayo, matukio ya ubakaji yalikuwa 2,984.

“Mtoto ni taifa la kesho, endapo atafanyiwa ukatili leo, je, kesho taifa hili litaongozwa na nani? Tamwa tunasisitiza hatua kali za kisheria na mabadiliko mengine ya kisera ili kumlinda mtoto dhidi ya ukatili,” alisema Reuben.

Aliwasihi wazazi, walezi kulipa uzito mkubwa suala la ulinzi kwa mtoto ili kuepusha ubakaji .

Aidha, alisema ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (Unicef) inaonyesha kuwa wabakaji wengi ni ndugu wa karibu ambao wanaishi ndani ya familia.

“Kupinga unyanyasaji, ubakaji na ulawiti wa watoto ni jukumu la jamii nzima na wakati umefika sasa kila mmoja kwenye nafasi yake awalinde watoto kwa kuripoti vitendo vya unyanyasaji vilivyofichika kwenye jamii yetu,” alisisitiza.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika kila Juni 16, na kauli mbiu ya mbiu ya mwaka huu ni “Mtoto ni msingi wa taifa endelevu tumtunze, tumlinde na kumwendeleza”.

Habari Kubwa