Matumizi plastiki marufuku taasisi za serikali

14Sep 2021
Ashton Balaigwa
KILOSA
Nipashe
Matumizi plastiki marufuku taasisi za serikali

SERIKALI imepiga marufuku matumizi ya kamba za plastiki, matumizi ya vifungashio vya plastiki ikiwamo magunia kwenye taasisi zake, badala yake watumie vifungashio vinavyotokana na mkonge unaozalishwa hapa nchini.

Maamuzi hayo ya Serikali yamekuja baada ya kubainika kamba hizo zinaleta athari kwa afya wa binadamu pamoja na uharibifu wa mazingira hapa nchini.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, katika mkutano wa pili wa wadau wa sekta ya mkonge hapa nchini, ulioshirikisha wakulima, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na wadau wanaolima zao hilo nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa aliiagiza Wizara ya Kilimo, kutoa tamko la kisera kwa ajili ya kuzuia matumizi ya kamba za plastiki nchini, ambazo zimebainika nyingi ni bandia na zinazalishwa kwa njia za panya.

Alisema amekuwa akipokea malalamiko ya muda mrefu kuhusu kuwapo kwenye soko kwa kamba hizo bandia za plastiki ambazo zimetengenezwa na viwanda bubu hapa nchini.

Hivyo aliiagiza Shirika la Viwango (TBS) kudhibiti kamba hizo katika soko na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kuhakikisha inazipiga marufuku kwa kuwa ni tishio  kwa mazingira.

Alisema pamoja na malalamiko hayo lakini matumizi ya mifuko ya plastiki imekuwa pia ikisababisha serikali kupoteza mapato yanayotokana na kodi.

Majaliwa alisema lengo la Serikali ni kuinua kilimo cha mkonge kwa kuongeza uzalishaji kutoka tani 37,000 za hivi sasa hadi tani 120,000 ifikapo mwaka 2025.

Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ikabidhi kwa Bodi ya Mkonge Tanzania, mashamba yote yaliyofutwa na Rais Samia Hassan Suluhu kwa ajili ya kugaiwa wananchi.