Mauaji wivu wa mapenzi yanavyoacha simanzi

26Jul 2021
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
Mauaji wivu wa mapenzi yanavyoacha simanzi
  • *Polisi, LHRC na wanasaikolojia wanena

MATUKIO ya ukatili wa mauaji, unajisi na ubakaji dhidi ya binadamu wengine yanaongezeka sababu kubwa ikitajwa ni wivu wa kimapenzi kiasi cha kugharimu maisha ya wengine na kuacha watoto yatima, ulemavu na uadui kati ya ndugu na ndugu au wanajamii.

Kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo, Nipashe imefanya utafiti kwa kuangazia matukio yaliyotokea kuanzia Juni mwaka 2020 hadi Julai mwaka huu, na kubaini kuwa matukio yaliongoza ni ukatili kati ya wapenzi na kwa mwaka jana, kulikuwa na matukio 75 huku mwaka huu yakiwa 56.

Aidha, matukio ya wivu wa kimapenzi yalikuwa 38 na kati yake mwaka 2020 yaliongoza yalikuwa 23 na mwaka huu 15, huku matukio ya ubakaji ( 27) ambayo ni 20 mwaka jana na saba mwaka huu.

Kwa mwaka jana idadi ya matukio kila mwezi kwenye mabano ni Juni (12), Julai (6), Agosti (13), Septemba (12), Oktoba (13) Novemba (11) na Desemba (8).

Kwa mwaka huu, Januari uliongoza kwa kuwa na matukio 14, ukifuatiwa na Aprili matukio tisa, Machi na Juni ulikuwa na matukio nane huku mwezi huu ambao umebakisha siku tano ukiwa na matukio 10 na Februari ukirekodi machache yaani manne.

TAKWIMU ZA POLISI

Julai 20, mwaka huu, Jeshi la Polisi nchini lilitoa takwimu za nchi nzima kuanzia Mei hadi Juni mwaka huu, zikionyesha watu 5,429 walikamatwa kwa kujihusisha na uhalifu.

Matukio ya mauaji yalikuwa 275 na kati yake wivu wa mapenzi ni 21 imani za ushirikina ni 23 na 231 sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujitafutia kipato kwa njia za kiuhalifu.

MWANASAIKOLOJIA

Mwanasaikolojia na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Magolanga Shagembe, akifafanua kwamba kiini cha matukio ya kuuana miongoni mwa wachumba na wanandoa yanayoripotiwa kwa wingi nchini inachangiwa na uchumba na ndoa nyingi kujengwa kwa msingi aliouita mbovu wa kukidhi haja ya kimwili.

“Uhusiano unavunjika kwa sababu yanajengwa katika msingi mbovu. Vijana wengi wanaingia katika mahusiano kwa lengo la kikidhi haja zao za kingono tu na siyo mapenzi ya dhati,” alibainisha.

“Ili uhusiano uwe na tija, ni lazima kuwe na vitu vya ziada vya kuwaunganisha wahusika, tofauti kabisa na kuishia kufanya mapenzi tu, mfano kushauriana mambo ya shule, kazi na maisha kwa ujumla,” alisema.

LHRC

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema kumekuwa na mwendelezo wa matukio ya ukatili na mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi, watu kujichukulia sheria mkononi na mengine yanayohusishwa na imani za kishirikina.

Alisema utafiti uliofanywa na LHRC mwaka 2019 ulibaini matukio takribani 12 ya mauaji ya wanawake, yaliyofanywa na wenza wao, huku matukio nane yakihusishwa na wivu wa kimapenzi.

Pia kwa mwaka 2020, idadi ya matukio ya mauaji ya wanawake yaliyofanywa na wenza wao, yaliongezeka hadi kufikia 32 huku 23 yakisababishwa na wivu wa mapenzi, na kutoa wito kwa wananchi kulinda haki wengine.

MWAKA JANA

Kwa mwaka jana, matukio yaliyoripotiwa ni Juni 2, mchungaji wa Kanisa la Mlango wa Ukombozi, Gairo mkoani Morogoro, Joseph Gervas (28), alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi.

Siku hiyo hiyo, watoto wawili wa miaka minne waliuawa mkoani Pwani na Shinyanga kwa kukatwa mapanga, wa kwanza chanzo ni wivu wa mapenzi kwa mke mkubwa Sofia Mariam (28) kukosa mtoto wakati mke mdogo ana mtoto, na wa Shinyanga chanzo hakikubainishwa.

Juni 3, watu watatu walishikiliwa Kinondoni kwa tuhuma za kumuua dereva teksi, Joseph Mwenda na kumzika maeneo ya karibu na Shule ya St. Mary’s Mbezi Makonde kisha kumwibia.

Siku hiyo hiyo, Justine Joseph mkazi wa Wilaya ya Kyerwa, alishikiliwa kwa tuhuma za kumuua mama yake kwa kumshambulia na kipigo, kumbana shingo hadi kufa, kwa madai ya kuto mhudumia mgonjwa ambaye ni baba yake.

Juni 14, Mahakama ya Mkoa wa Lindi ilimhukumu Kasimu Chilimba (18), mkazi wa Kata ya Nyengedi kuchapwa viboko 12 baada ya kukutwa na kosa la kumbaka mwanafunzi.

Juni 16, mkazi wa Kimara mkoani Dar es Salaam, Erick Bubelwa, alishikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua mke wake, Mercy Mkambala (30) chanzo wivu wa kimapenzi.

Juni 18, 2020, mkazi wa Bunda jina lake halikubainishwa, alishikiliwa kwa tuhuma za kuwazalilisha kijinsia na kuwabaka mfululizo watoto wake watatu na kumpa mimba wa miaka 13.

Juni 19, aliyekuwa mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chisegu, Masasi mkoani Mtwara Mohamedi Mboloma alikutwa amejinyonga msituni, baada ya kutoweka nyumbani kwake siku tatu.

Juni 20, walimu katika kijiji cha Chihwanga, Kata ya Itaragwe wilayani Gairo, mkoani Morogoro, mwalimu mmoja aliuawa na mwingine kujeruhiwa kwa madai ya wivu wa mapenzi.

Juni 23, baba mmoja mkazi wa Bunda, alidaiwa kumbaka mtoto wake wa kumzaa kwa ahadi ya kumpa Sh. 5,000.

Juni 25, mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi Kange, kilichopo mkoani Tanga Waziri Ramadhan, alituhumiwa kwa kumuua mwanafunzi mwenzake Hussein Daudi, baada ya kumkuta kwenye chumba cha rafiki yake wa kike.

Juni 30, wafanyakazi wanne wa kiwanda cha uchenjuaji Madini ya Dhahabu (Plant) katika mgodi mdogo wa Mtambalale, kijiji cha Wisolele, wilayani Kahama waliuawa kwa kucharanga na mapanga na watu wasiojulikana, na sababu ya tukio hilo ni kutaka kupora mali.

Julai Mosi, Sinoni mkoani Arusha, ndugu wawili wa familia moja walituhumiwa kumuua mdogo wao, Mandela Malisa kwa madai ya kumkuta amelala kwenye chumba cha baba yao mzazi ambaye ni marehemu, chanzo kikidaiwa kugombania nyumba ya urithi.

Julai 9, Juma Kisinza (50) alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa miaka 13.

Julai 8, Chalinze mkoani Pwani, mfanyakazi za ndani Yasini Abdalla (35) aliuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kudaiwa kuwaua watoto wawili wa familia moja na kumjeruhi mama yao chanzo kutoelewana.

Julai 10, Daria Frank (55) mkazi wa Mamba wilayani Moshi alishikiliwa na polisi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kumuunguza na moto mtoto wa miaka sita.

Julai 21, Alistides Crizostom (40) mkazi wa Karagwe mkoani Kagera alishikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mke wake Donina Alistides (53), baada ya kufumania na mwanaume mwingine.

Julai 31, mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kilango, Kahama mkoani Shinyanga alidaiwa kubakwa siku ya mkesha wa harusi.

Agosti 4, kijana Ulandi Dotto (28) mfugaji mkazi wa Mbarali mkoani Mbeya alifariki dunia baada ya kupigwa risasi na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) baada ya kupitisha mifugo yake ndani ya eneo la hifadhi.

Agosti 6, mfanyakazi za ndani Magige Thomas (21) mkazi wa Tarime mkoani Mara, alihukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la ulawiti.

…Itaendelea Kesho