Mavazi nusu utupu yawachefua wazee

26Jun 2022
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe Jumapili
Mavazi nusu utupu yawachefua wazee

​​​​​​​WAZEE wa Mtaa wa Dome, Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga wameeleza kuchefuliwa na mavazi ya nusu utupu yanayovaliwa na wasichana huku wakieleza kuwa yamekuwa ‘yakiwatega’ wanaume na kusababisha kuwafanyia vitendo vya ukatili, ukiwamo ubakaji.

Hayo yalibainishwa na wazee hao juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mtaa wa Dome uliokuwa na lengo la kutoa elimu ya kupiga vita biashara na matumizi ya dawa za kulevya, vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuimarisha ulinzi na usalama.

Mmoja wa wazee hao, Robert Mwelo, alitaja moja ya sababu ya kuwapo kwa matukio ya ukatili wa kijinsia ni mavazi ya nusu utupu yanayovaliwa na baadhi ya wasichana ambayo huhamasisha wanaume na mwishowe kuwabaka.

"Mavazi ya wasichana wetu ya nusu utupu ndiyo chanzo cha matukio haya ya ukatili. Unajua wanawake ni kama sumaku, wewe unamwona binti kavaa nusu utupu, halafu anatembea huku akitingisha mwili, nikimwona ninaanza kufikiria nimvae nini, maana ananitega. Kwa mavazi haya ya nusu utupu, mtawafunga jela wanaume wengi," alionya.

Mratibu wa Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi Wilaya ya Shinyanga, Brighton Rutajama, alisema jamii inapaswa kuendelea kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutoa taarifa dhidi ya matukio hayo na ushahidi mahakamani ili wahusika wachukuliwe hatua.

Mratibu wa Polisi Jamii Wilaya ya Shinyanga, Osward Nyorobi, aliwataka wazazi mkoani humo kujenga tabia ya kukagua watoto wao kila mara kabla ya kulala ili kuona kama hawajafanyiwa vitendo vya ukatili.

Pia aliwataka wawe makini na wageni wanaokwenda kwenye nyumba zao kwa kuwa matukio mengi ya ukatili wa kijinsia hufanywa na watu wa karibu.

Mwenyekiti wa Mtaa huo wa Dome, Solomoni Najulwa, alisema wameendesha mkutano huo ili kutoa elimu kwa wananchi ili kuacha vitendo vya uhalifu pamoja na ukatili wa kijinsia.

Habari Kubwa