Mavunde ajitamba kuing’arisha Dodoma akishinda ubunge

06Sep 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe Jumapili
Mavunde ajitamba kuing’arisha Dodoma akishinda ubunge

Mgombea Ubunge Jimbo la Dodoma mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, amezindua kampeni zake, huku akiwaahidi kuing’arisha Dodoma kimaendeleo kwenye nyanja mbalimbali.

Mgombea Ubunge Jimbo la Dodoma mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde.

Akizungumza na wananchi wa jimbo hilo, kwenye viwanja vya shule ya msingi Chang’ombe, Mavunde jana amesema miaka mitano ya kwanza ambayo wananchi wameshuhudia Dodoma ikikua kwa kasi ilikuwa ya yeye kujifunza lakini wakimchagua tena watashuhudia makubwa kwenye sekta ya afya, elimu, maji, miundombinu na michezo.

Amebainisha kuwa katika sekta ya elimu atahakikisha wanafunzi wanasoma kisasa na atatoa komputa kwa shule zote za msingi na sekondari kwenye jimbo hilo.

“Katika ubunge wangu wa miaka mitano nimejenga shule mbili za sekondari na kujenga madarasa katika shule kadhaa za msingi na sekondari, na endapo wananchi mtanichagua tena nitaongeza kasi ya kujenga shule hususani katika maeneo ambayo wanafunzi wanalazimika kutembea muda mrefu kufuata elimu,”amesema.

Aidha, amesema endapo akichaguliwa hatasubiri fedha za Serikali kuu pekee bali atatafuta wadau ili kusaidia kuharakisha maendeleo kwa wananchi ikiwamo upatikanaji wa maji ya uhakika na yanayotosheleza jiji hilo.

Habari Kubwa