Mavunde awapa somo vijana kuhusu uchaguzi

13Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mavunde awapa somo vijana kuhusu uchaguzi

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, amewataka vijana kushiriki katika uchaguzi mkuu na kutumia haki yao kikatiba katika hali ya amani na utulivu.

Mavunde alitoa kauli hiyo jana jijini hapa alipokuwa akitoa tamko la serikali la Siku ya Vijana Duniani.

“Lazima tutambue umuhimu huu wa uchaguzi kwa kuwawezesha vijana wetu kwenda kupiga kura kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa. Hii ni haki yao kikatiba na kamwe wasitumiwe vinginevyo,” alisema.

Aliwataka kutambua kuwa hakuna taifa lolote duniani lenye maendeleo bila amani kwa kuwa ni nguzo kubwa ya umoja na demokrasia ya kweli nchini.

Pia alisema serikali ya awamu ya tano imetoa fursa kwa vijana na kuchangia kuwepo na mwamko mkubwa wa wao kushiriki kwenye siasa za uongozi.

“Mwaka huu umekuwa mwaka wa kipekee ambao umeleta mwamko wa vijana kugombea na asilimia 90 waliojitokeza ni vijana, wamebadilika na hawakai tena nyuma, wapo mbele katika kulijenga taifa lao,” alisema.

Akizungumzia kuhusu siku hiyo, Mavunde alisema Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2020 inaeleza kuwa idadi ya vijana ni bilioni 1.8 ambayo ni sawa na asilimia 24 ya watu wote ambao ni bilioni 7.5.

Hata hivyo, alisema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakadiria kuwa ifikapo mwaka 2035, idadi ya vijana itafikia asilimia 34.5 ambayo ni sawa na watu milioni 19.9 ya Watanzania milioni 57.6.

Kwa upande wa nguvu kazi, Mavunde alisema Shirika la Kazi Duniani (ILO) linabainisha kuwa uelekeo wa nguvu kazi duniani mwaka 2020, asilimia 41.2 inatokana na vijana huku Tanzania nguvu kazi asilimia 56 ni vijana.

Alitaja mambo mbalimbali yaliyofanyika nchini kwa ajili ya vijana ikiwemo programu ya kukuza ujuzi wa nguvu kazi ambapo vijana 28,941 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi kwa fani za ufundi stadi wa ushonaji nguo, useremala, uashi, uchongaji vipuri, umeme, upishi na huduma za hoteli.

Pia alisema serikali imeanzisha programu ya stadi za maisha kwa vijana walio nje ya shule kwa lengo la kuhakikisha kuwa vijana wanakabiliana na changamoto zitokanazo na shinikizo rika.

Habari Kubwa