Mawakili watano kuwatetea vijana waliofungwa maisha

28Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mawakili watano kuwatetea vijana waliofungwa maisha

MAWAKILI watano wanakusudia kukata rufani kupinga hukumu ya kifungo cha maisha jela, iliyotolewa wiki iliyopita na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, dhidi ya washtakiwa wanane kwa kosa la kuchoma Kituo cha Polisi cha Bunju A jijini Dar es Salaam.

Wakili Jebra Kambole ni miongoni mwa mawakili waliojitosa kutaka rufani kuwachomoa vijana hao ambao hukumu dhidi yao iliibua vilio, simanzi na taharuki kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Vijana hao walikuwa wanakabiliwa na makosa sita yakiwamo ya kufanya mkusanyiko usio halali, kuharibu mali, kumwagia petroli na kuchoma moto Kituo cha Polisi cha Bunju A, mwaka 2015.

Akizungumza na Nipashe jana, Wakili Kambole alisema tayari wameshapeleka notisi ya kusudio hilo Mahakama Kuu.

"Kwa sasa tumeshatoa notisi ya kusudio la kukata rufani maana kikawaida inatakiwa utoe notisi ndani ya siku 10, baada ya hapo, utaratibu mwingine utafuata," Kambole alisema.

Ijumaa iliyopita, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliwahukumu kifungo cha maisha jela washtakiwa wanane kati ya 18 baada ya kutiwa hatiani katika kesi ya kuchoma Kituo cha Polisi cha Bunju A.

Awali kesi hiyo ilikuwa na washtakiwa 35, lakini baadaye Mahakama iliwaachia huru washtakiwa 17 na kubaki 18 na kati yao, wanane ndiyo walitiwa hatiani Ijumaa iliyopita, huku 10 wakiachiwa huru.

Waliokutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha ni Ramadhan Said (22), Veronica Ephraim (32), Yusuph Sugu (40), Juma Kozo (32), Rashid Liwima (29), Baraka Nkoko (23), Abuu Issa (36) na Abraham Mninga (23).

Walioachiwa huru ni Hamis Ndege (37), Anthony Mengenya (28), Rehema Hussein (32), Rajabu Ally (25), Gubila Temba (51), Mariam Honza (44), Mrisho Majaliwa (30), Seleman Gwae (33), Ally Athuman (24) na Rajab Ally (25).

Habari Kubwa