Mawaziri watatu wajadili soko la minofu ya Samaki Nje ya Nchi

02Jun 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Mawaziri watatu wajadili soko la minofu ya Samaki Nje ya Nchi
  • Ni kutoka Wizara tatu wapo pia Makatibu wakuu pamoja na Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara

Ili kuhakikisha biashara ya minofu ya samaki katika masoko ya nje ya nchi inakuwa endelevu, Mawaziri wa Wizara tatu, Makatibu wakuu pamoja na Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara wamekutana kwa ajili ya kuweka mikakati ya pamoja.

Kikao hicho kilichofanyika mkoani Mwanza na kuhudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Makatibu Wakuu wa Wizara husika akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Rashid Tamatamah,Wakuu wa Mikoa hiyo akiwemo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella ambaye alikuwa mwenyeji, na wataalamu wa sekta husika.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amesema lengo la kikao hicho ni kuweka mikakati ya pamoja itakayowezesha biashara iliyoanza Mei, 12, mwaka huu ya kusafirisha samaki kwenye masoko ya nje kutokea uwanja wa ndege wa Mwanza inakuwa endelevu.

Kamwelwe, amesema mpango huo utawezesha kukuza uchumi wa wananchi wa Kanda ya Ziwa  pamoja na Taifa kwa ujumla, watakao pata faida moja kwa moja katika mnyororo huo wa biashara ni wazalishaji wa samaki pamoja na taasisi ambazo zitakusanya tozo kutokana na huduma zitakazotolewa.

Amesema taasisi hizo ni pamoja na Mamlaka ya  ya Viwanja vya Ndege, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Anga na Mamlaka ya hali ya hewa ambapo pale itakapowezekana  waongeze aina zingine za bidhaa au mazao yanayoweza kusafirishwa kwenda masoko ya nje ya nchi ili kuongeza wigo wa wanufaika kama vile wanavyojua kuwa ukanda huu ni wa mifugo ikiwemo ng'ombe na  mbuzi.

" Kwa maelekezo hayo  niliagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi akutane na wenzake wa Mifugo na Uvuvi pamoja na wa Viwanda na Biashara ili wafanye uchambuzi na kushauri namna bora ya kushirikiana katika maeneo yanayotuhusu na kuifanya biashara ya usafirishaji minofu ya samaki kutokea katika kiwanja cha ndege cha Mwanza iwe endelevu pamoja na kuhakikisha tunakuwa na ndege yetu ya mizigo ambayo itabeba mizigo/minofu ya samaki ya kudumu na uhakika," alisema Kamwelwe.

Aidha alitumia fursa hiyo kueleza kuwa tangu kuanza kwa safari za kubeba samaki kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza kwenda masoko ya Ulaya kumekuwa na jumla ya safari nne ambapo kati ya hizo ni tatu zilikuwa za shirika la ndege la Rwanda(RwandAir) na moja ya shirika la ndege la Ethiopia (Ethiopian Airline).

Hata hivyo alisema,katika safari hizo kumejitokeza changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na mashirika hayo ya ndege kupitia maofisa wao wa masoko pamoja na kuwepo hoja mbalimbali zinazohitaji kutafutiwa ufumbuzi zilizowasilishwa na wazalishaji wa samaki.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Rashid Tamatamah, amesema Serikali imeanzisha mchakato wa kusafirisha minofu ya samaki moja kwa moja kutoka Mkoani Mwanza hadi nje ya nchi hivyo wasinge penda uishie katikati ndio maana wameamua kuwa na kikao hicho baada ya changamoto ambazo zimejitokeza  na zisipotatuliwa zinaweza kufanya mashirika ya ndege yanayokuja kuchukua samaki yasitishe. 

" Kila Wizara tumegawana majikumu mbalimbali katika kutatua hizo changamoto zilizojitokeza  katika kikao cha pili kitakachofanyika Dodoma kila Wizara inapaswa kuleta mrejesho wa  wapi walipofikia katika kutatua changamoto hizo,Wizara yetu kwa muda wa miaka miwili iliopita viwanda vingi vilisimamisha uzalishaji," nakuongeza

"Lakini sisi kwenye Wizara yetu mchakato ambao tumeufanya ni oparesheni ambayo baada ya miaka miwili imezaa matunda,sasa hivi samaki wameongezeka kiasi kwamba sasa viwanda vinafanya uzalishaji kwa kiasi kikubwa ambapo changamoto kubwa kwa sasa ni masoko ambayo moja ya kuhakikisha kupata masoko ni hiyo ya kusafirisha nje na mwaka jana walianza mchakato wa kuhamasisha wachakataji wadogo kuanzisha vikundi na kugandisha samaki na kuuza sehemu mbalimbali nchini," amesema Dk.Tamatamah.

Pia aliwataka watu wa Kanda ya Ziwa kuacha kutumia zana haramu kwani zimesaidia kuongeza samaki ili sasa wajikite katika kutafuta masoko.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amesema asilimia  katika masoko ya nje zinapokwenda samaki wanaopatikana katika ziwa Victoria kwa nchi ya Tanzania wanaoenda ni asilimia chache lakini ndipo kwenye asilimia zaidi ya 50 ya ziwa hilo ndio jambo ambalo wanatoka nalo hapo kwenda kujiuliza kwanini wao ndio wana eneo kubwa la ziwa,mazao mengi ya samaki na maziwa yote yanayotema maji lakini upelekaji wa samaki nje ni mdogo.

"Tupo jiuliza swali hilo tunakwenda kuangalia na fursa hii iliyojiyokeza ya Mwanza kuwa mji wa kusafirisha samaki moja kwa moja kwenda Ulaya,tuweke na brandi ya kujitangaza kuwa chanzo cha samaki wa Ziwa Victoria wanatoka kwetu pia tujue kiwango gani kinacho hitajika katika masoko ya nje,kwani wa viwanda  lazima wawe watu kutoka nje hapana tuanze kutengeneza viwanda vidogo na ambavyo vinakidhi mahitaji na viwango vya masoko ya Ulaya  na  afya," amesema Malima.

Habari Kubwa