Mawaziri waliotaabika 2018

28Dec 2018
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Mawaziri waliotaabika 2018

MWAKA 2018 ambao umebakiza siku tatu kumalizika haukuwa mzuri kwa mawaziri wanne walioongeza idadi ya mawaziri waliotumbuliwa tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani mwaka 2015, kufikia tisa.

Aidha, mawaziri wanane walipitia misukosuko ambayo ilisababisha baadhi yao kutajwa hadharani na Rais John Magufuli kuwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kadiri ya maelekezo aliyoyatoa.

Mawaziri hao walitumbuliwa kwa nyakati tofauti, na Rais Magufuli alieleza sababu za kumtumbua kila mmoja wao wakati wa hafla ya kuapishwa kwa wengine wapya.

Waliotumbuliwa

Waziri wa kwanza kukumbwa na fagio hilo mwaka huu ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, aliyetumbuliwa Julai Mosi, mwaka huu, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma.

Aidha, Julai 2, mwaka huu wakati wa kuapishwa Waziri mpya Kangi Lugola, Rais Magufuli alitaja sababu za kutumbuliwa kwa Dk. Mwigulu, kuwa ni kushindwa kutekeleza Azimio la Bunge kuhusu kufungwa kwa alama za kielektroniki za utambuzi wa alama za vidole katika vituo 108 vya polisi uliofanywa na kampuni ya Lugumi kwa gharama ya Sh. bilioni 37.

Nyingine ni mkataba tata wa manunuzi ya magari 777 ya polisi, kushughulikia changamoto zinazolikabili Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ajali barabarani, usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali, kutopandishwa vyeo kwa askari, masuala ya wakimbizi na kuhakikisha wafungwa wanazalisha mali.

Waziri wa pili kuonja shubiri mwaka huu ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Susan Kolimba, aliyetumbuliwa Septemba 26, mwaka huu, kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Damas Ndumbaro.

Wakati wa kuapishwa Dk. Ndumbaro, Rais Magufuli alieleza bayana kwamba haridhishwi na mambo yanavyokwenda kwenye wizara hiyo na alimtetea Waziri Augustino Mahiga kwamba amekuwa na majukumu mengi ya kumwakilisha nje ya nchi, lakini naibu wake alipwaya kusimamia majukumu mengine.

Siku chache baadaye, Rais Magufuli aliwatumbua mawaziri wawili kwa kushindwa kutekeleza vyema majukumu yao kwenye wizara zao ikiwamo kushindwa kusimamia taasisi na bodi mbalimbali ambazo zinawajibu wa kuangalia bei za mazao ya wakulima.

Waliotumbuliwa Novemba 10, mwaka huu ni aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Joseph Kakunda, ambaye kabla alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Mwingine aliyekumbwa na fagio la chuma ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo Dk. Charles Tizeba, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Japhet Hasunga, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

Akizungumza Novemba 12, wakati wa kuapishwa kwa viongozi mawaziri wapya, Rais Magufuli aliwapongeza kwa kuhudhuria na kushuhudia uwapishwaji wa wenzao.

“Ninawashukuru sana Dk. Tizeba na Mwijage, ninyi ni wazalendo, mmeonyesha ushujaa wa pekee, mmekuja mmejua hizi kazi ni temporary (za muda) kwa sababu hata maisha ni temporary (ya muda), mmejitahidi kufanya kwa wakati wenu, waje wengine msisite kuwasaidia,” alisema.

Waliopitia wakati mgumu

Desemba 21, mwaka huu, Rais Magufuli alimuumbua hadharani Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, kwa kupenyeza majina 11 ya ndugu zake aliotaka waajiriwe ndani ya Jeshi la Polisi nchini.

Desemba 14, mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inayoongozwa na Kangi Lugola, ilijikuta matatani baada ya wizara yake kutoa barua ya kuelekeza mabadiliko matumizi ya bendera, nembo na wimbo wa taifa.

Siku chache baada ya barua hiyo kuvuja na kuandikwa na vyombo vya habari, Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilitoa taarifa ya kufuta barua hiyo kwa kuwa ina maelekezo yanayoathiri uzalendo wa Watanzania na italeta mkanganyiko wa alama na rangi zilizomo kwenye bendera ya taifa.

Waziri mwingine aliyepitia misukosuko ni wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ambaye aliingilia sakata la kontena zilizozuiliwa bandarini zilizokuwa na jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutokana na kutolipiwa kodi.

Katika sakata hilo Waziri Mpango alisema ni lazima kodi ilipwe, lakini Makonda alisema ataisemea Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na waziri wao kwa Rais kwa kuwa mali zilizokuwa ndani ya kontena hizo ni za samani za ofisi za walimu wa mkoa huo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kigwangalla, alipata ajali Agosti 4, mwaka huu, eneo la Magugu mkoani Manyara na kuvunjika mkono na kuumia sehemu mbalimbali za mwili.

Katika ajali ambayo ilisababisha kifo cha Ofisa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Hamza Temba, Waziri huyo alihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alitibiwa na kuruhusiwa.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Isack Kamwele, ambaye alijikuta katika misukosuko baada ya kutokea kwa ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyosababisha vifo vya mamia ya watu.

Rais Magufuli aliamua kuvunja Bodi ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) hali iliyomlazimu waziri huyo kupiga kambi kwa wiki mbili katika kisiwa cha Ukara ambacho watu wake wengi walipoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea Septemba 21, mwaka huu.

Mawaziri waliong’ara na kupongezwa

Novemba 12, alipokuwa akiwaapisha mawaziri wapya, Rais Magufuli alimmwagia sifa Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, kuwa anafanya kazi nzuri kwa kuwa yuko kila mahali na amejenga vituo vya afya zaidi ya 300, hospitali za wilaya zaidi ya 67.

Jafo alipanda na kuwa waziri kamili baada ya aliyekuwa Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, kuondolewa katika nafasi hiyo mwaka jana.

Waziri mwingine ambaye wizara yake ilikuwa na utulivu na waziri husika kutopataka misukosuko ni wa Elimu, Sayansi, Tekonolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ambaye aliteuliwa kuongoza wizara hiyo tangu mwaka 2015 na kudumu hadi sasa.

Wengine ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, aliyepanda kutoka kuwa Naibu Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini na Waziri wa Madini, Angela Kairuki, aliyeteuliwa Oktoba mwaka 2017.

Mwingine ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ambaye alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na baada ya kuonekana anafanya vizuri aliteuliwa kuwa Waziri kamili na mara kadhaa Rais amekuwa akimpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya.

Waziri mwingine ambaye mambo yamemwendea vizuri tangu alipoteuliwa ni wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, ambaye alianza na Rais Magufuli tangu aingie madarakani mwaka 2015.

Lukuvi ameonekana kuimudu wizara hiyo na kumfanya Rais amwache kwenye wizara hiyo kutokana na kazi ya kuzunguka nchi nzima kutatua migogoro ya ardhi na kuchukua mashamba yasiyoendelezwa.

Waziri ambao hawakupata misukosuko mwaka huu ni Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Serikani bungeni.

Mhagama amekuwa akisimamia nidhamu bungeni na mara kadhaa wabunge hasa wa upinzani wanapotumia lugha za kuudhi dhidi ya serikali amekuwa akipambana nao kwa kutumia Kanuni za Bunge.

Mawaziri ambao hawavumi lakini wamo

Kwa mwaka 2018 waziri ambaye wizara yake haikuwa na mikiki mikiki wala kuvuma kwenye vyombo vya habari ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi.

Habari Kubwa