Rais Mwinyi ameyasema hayo Ikulu ya Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi na kuongeza kuwa uongozi wake unajipanga kutimiza ahadi alizotoa kwa wananchi.
Pia Rais Mwinyi ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa kipaumbele katika kuimarisha Uchumi wa Bahari kuu hasa Uchumi wa bluu kama chanzo mbadala cha mapato kitakachosaidia kukuza uchumi na kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetoa kipaumbele katika kuimarisha Uchumi wa Bahari kuu hasa Uchumi wa bluu kama chanzo mbadala cha mapato kitakachosaidia kukuza uchumi,” amesema Dkt. Mwinyi

Katika tukio jingine, Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje umekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye amesisitiza kuwa uchumi wa bluu ni muhimu sana kwa maendeleo ya Zanzibar hivyo ni muhimu kwa Serikali zote mbili (Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) kulinda mipaka yake ya bahari ambapo pia ulinzi huo utasaidia kuzuia na kupambana na uingizwaji wa dawa za kulevya hapa nchini.
“Naamini kabisa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tukishirikiana katika kuimarisha ulinzi wa baharini itasaidia kupunguza uingizwaji wa dawa a kulevya hapa nchini,” amesema Maalim Seif


Kwa upande wake Prof. Palamagamba Kabudi ameupongeza uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kwa hatua ulizozichukua katika kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu visiwani humo na kwamba uwepo wa amani na utulivu utachangia kuleta maendeleo haraka kwa wananchi wa Zanzibar.
“Zanzibar imetulia na uchumi wake umezidi kuimarika sote ni mashahidi wa ongezeko la watalii hapa Zanzibar hii ni ishara ya kuwa na amani na utulivu, na jambo hili linachangia kukua kwa uchumi wa Zanzibar,” amesema Prof. Kabudi
.jpeg)
Mbali na kukutana na Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais, pia Uongozi huo umekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla ambapo wamejadili masuala mbalimbali ya maendeleo yanayohusu Tanzania Bara na Zanzibar hususan yanayohusu Muungano.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi katika ziara yake ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, William Olenasha pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.