Mbarawa aibua madudu ujenzi mwendokasi

17Sep 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Mbarawa aibua madudu ujenzi mwendokasi

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya mwendokasi kutoka Kariakoo hadi Mbagala, kurudia kipande cha kilometa mbili kilichojengwa chini ya kiwango ndani ya miezi mitano.

Aidha, ameagiza makandarasi wanaofanya makosa kama hayo zaidi ya mara moja kunyimwa tenda zingine za serikali, ili kutoa funzo la kuacha kucheza na miradi ya umma.

Waziri Mbarawa alitoa agizo hilo jana, alipofanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara za mkoani wa Dar es Salaam, zikiwamo ya Mbagala na Kimara hadi Kibaha.

“Ujenzi huu uko chini ya kiwango, naomba mkandarasi afumue kipande chote cha kilometa mbili na kujenga upya. Hapa kwa mtu wa kawaida unaweza kuona ni kitu cha kawaida, lakini baada ya magari kupita tatizo litazidi kuwa kubwa. Kama tusingeona, tungekuwa tumeliwa,” alisema Prof. Mbarawa.

Alisema barabara hiyo inajengwa kwa awamu mbili ambayo ya kwanza inagharimu Sh. bilioni 217 na awamu ya pili kwa Sh. bilioni 45 na kwamba kazi inaenda vizuri.

Kuhusu makandarasi wanaofanya kazi chini ya kiwango, alisema wanyimwe tenda ili kuwajengea nidhani ya kufanya kazi kwa uadilifu.

“Mkandarasi akirudia kosa kama hili, akarudia tena maeneo mengine mawili, akileta maombi ya tenda tupilieni mbali maombi yake,” alisema waziri.

Alisema serikali itanunua mitambo ya skana za kufanya ukaguzi wa barabara kwa ajili ya kubaini ubora baada ya kujengwa na kwamba ilishanunua mtambo mmoja wa kukagua barabara, lakini ulikaa muda mrefu bila kufanya kazi, hivyo wataongeza mingine na kugawa kanda zote nchini.

Akizungumzia mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Rogatus Mativila, alisema awali mradi huo ulitakiwa kukamilika mwaka huu, lakini utakamilika Machi mwaka 2023.

Alisema ulikuwa ukamilike mwaka huu miezi 47 tangu ujenzi uanze 2018, lakini ulichelewa kwa sababu za kimenejimenti.

Alitaja sababu ya barabara kuharibika kabla ya kuanza kutumika, alisema mchanga uliotumika kujengea ulikuwa na udongo wa mfinyanzi ndio sababu ya kuanza kupata ufa na matobo madogo madogo.

Awali Waziri Mbarawa akikagua ujenzi wa barabara ya njia nane kuanzia Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa Kilometa 19.2, alisema ujenzi huo unaogharimu Sh. bilioni 161, umefikia asilimia 94.

Aliwataka makandarasi kumaliza kazi zilizobaki ambazo ni ujenzi wa madaraja ya kuvukia abiria kituo cha Mbezi Luis na Kwa Yusuph, ufungaji wa taa za kuruhusu magari, ujenzi wa barabara ya kuingia kituo cha mabasi cha Magufuli na ujenzi wa kituo cha daladala Kibamba.