Mbarawa avunja bodi ya Chaliwasa, Dawasa yakabidhiwa jukumu

15Jan 2020
Frank Monyo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mbarawa avunja bodi ya Chaliwasa, Dawasa yakabidhiwa jukumu

WAZIRI wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amevunja Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) na kuiunganisha na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) tangu Januari 11,2020 ili kuongeza ufanisi katika maeneo ya kihuduma.

waziri wa maji profesa makame mbarawa.

Kauli hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo baada ya kumaliza ziara ya kukagua miradi ya maji inayoendeshwa na Dawasa iliyopo maeno ya Bunju, Mabwepande, Salasala na Changanyikeni.

Profesa Mkumbo amesema Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam ulikuwa na mamlaka mbili za maji ambazo ni Dawasa kwa Dar es Salaam na Pwani na Chaliwasa ambayo Ilikuwa na jukumu la hudumia maeneo ya Chalinze lakini ilikuwa inakabiliwa na changamoto kubwa kiuendeshaji.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo akiongozana na Afisa Mtendaji Mkuu Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja kukagua mradi wa kituo cha kusukuma maji kilichopo Bunju wakati wa ziara ya kukagua miradi ya Dawasa.

“Kutokana na taratibu za wizara za kuunganisha mamlaka za maji ili kuboresha uendeshaji na kuongeza tija, Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa amefanya uamuzi wa kuinganisha Mamlaka yetu ya Chalinze (Chaliwasa) na Dawasa tangu tarehe 11, Januari 2020 Mamlaka ya Chalinze hii ipo chini ya Dawasa,” amesema Mkumbo na kuongeza kuwa;

 

“Kwa maana hiyo Mh. Waziri amevunja Bodi ya Mamlaka ya Maji  Chaliwasa ambapo kwa sasa itaendeshwa na Bodi ya Dawasa iliyo chini ya Jenerali Mstaafu Davis Mwamnyange ambayo ni bodi makini na inafanya kazi yake ipasavyo,” amesema Mkumbo

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo kwenye tangi la kuhifadhia maji lililopo Salasala jijini Dar es salaam.

Ameongeza kuwa Chalinze wanakabiliwa na changamoto kubwa mbili, ya kwanza hawana uwezo wa kusimamia uendeshaji kwa maana ya kulipia umeme na ya pili ni kukosa uwezo wa kununua madawa ya kusafishia maji ambapo kwa kiasi kikubwa walikuwa wanategemea kutoka Dawasa.

 

“Dawasa ni mamlaka kubwa na inakusanya fedha nyingi ambazo zinawawezesha kujiendesha, tumetoka hapo Tegeta peke yake Dawasa inakusanya zaidi ya bilioni 1 na ndio inaongoza kuliko mamalaka nyingi hapa Tanzania na kwa sasa nchi nzima tunakusanya zaidi ya bilioni 23 kwa mwezi katika pesa hiyo bilioni 10 hadi 11 inakusanywa na Dawasa peke yake,” amesema na kuongeza kuwa;

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

A post shared by Nipashe (@nipashetz) on Jan 14, 2020 at 3:41am PST

“Kwa maana hiyo nusu ya mapato ya mamalaka za maji Tanzania yapo Dar es Salaam kwahiyo tunataka watumie “manguvu” yao haya wakatusaidie Chalinze kulipa umeme na gharama nyingine za uendeshaji ili serikali iweze kufanya mambo mengine makubwa,” amesema Mkumbo

Amesisitiza kuwa Dawasa inatekeleza miradi mingi katika maeneo ya Chalinze kwa maana hiyo baada ya kuiachia iliyokuwa bodi ya Chaliwasa ifanye kazi hiyo, Waziri aliona ni bora kuiweka mamlaka hiyo chini ya Dawasa ili kutoa nafasi kwa serikali kufanya mambo mengine.

Habari Kubwa