Mbarawa awatoa hofu wananchi Kigoma ujenzi barabara

18Jan 2022
Adela Madyane
Kigoma
Nipashe
Mbarawa awatoa hofu wananchi Kigoma ujenzi barabara

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Kigoma, mradi wa ujenzi wa barabara inayoanzia kijiji cha Mnanila wilayani Buhigwe mpaka Kabingo wilayani Kakonko kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 260.6 utaendelea kutekelezwa kama ilivyopangwa.

Ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo yenye thamani ya zaidi ya Bil. 300/-

Aidha, amewatoa hofu wananchi na kusema serikali itahakikisha inakamilisha ujenzi wa barabara hiyo hadi kufikia Oktoba 2023.

"Kumekuwa na kauli za baadhi ya watu kuwa mradi utasimama naomba niwahakikishie Raisi wetu Samia Suluhu Hassan, ameshatoa fedha za utekelezaji wa barabara hii na changamoto kubwa ni upatikanaji wa saruji jambo ambalo linashughulikiwa na ujenzi utaendelea wala hautasimama," amesema Mbarawa.

Mbarawa amesema wizara itashirikiana na wizara zingine kwa ajili ya kuangalia namna nzuri ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara katika suala la msamaha wa kodi kwa baadhi ya vifaa vya ujenzi ili kurahisisha utekelezaji wa miradi kwa wakati.

Hata hivyo, amemtaka mkandarasi mshauri wa mradi pamoja na ofisi ya Wakala wa Barabara (TANROADS) Kigoma kuhakikisha wanasimamia kwa karibu ujenzi wa barabara hiyo na uwe wa kiwango kinachokubalika pamoja na kumaliza kwa wakati kulingana na mkataba.

Naye, meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, amemhakikishia Waziri kwamba pamoja na changamoto za mvua kasi ya ujenzi iliyofikiwa inaendana na muda, hivyo ujenzi huo utakamilika kwa wakati na kwamba wanachi wa mkoa wa Kigoma watakabidhiwa barabara hiyo kwa muda uliopangwa.

Akizungumza kwa upande wa wananchi, Elias Karova, dereva taxi anayefanya safari zake Mnanila- Kasulu, amesema upatikanaji wa barabara ya lami utasadia kupunguza ajali pamoja na matumizi ya mafuta, na kuiomba serikali kuwatengenezea barabara za mchepuko wakati ujenzi wa barabara kuu ukiendelea ili kupunguza uharibifu wa magari yao.

Habari Kubwa