Mbaroni kwa madai kumwingizia chupa sehemu za siri mwanamke

22Nov 2022
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
Mbaroni kwa madai kumwingizia chupa sehemu za siri mwanamke

WATU wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Manyara kwa tuhuma za kumwingizia chupa ya bia kwenye njia ya haja kubwa mhudumu wa baa katika mji wa Mirerani, baada ya kumbaka na kumwingilia kinyume cha maumbile.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kumfanyia ukatili mhudumu huyo (jina limehifadhiwa), walipomaliza kunywa naye bia na pombe kali katika eneo la Songambele katikati ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani, walimchukua na kwenda kutimiza dhamira yao katika eneo la Kazamoyo.

 

Jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP) George Katabazi, aliwataja wanaoshikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na ukatili huo ni Frank Batezi na Nico Ngowo, wote wakazi wa Mirerani.

 

"Hawa watuhumiwa wawili walishirikiana na wenzao wengine wawili kufanya ukatili huo na baada ya kumaliza walichoamua kufanya walikimbia. Lakini kwa sababu serikali ina mkono mrefu, watuhumiwa hao wawili walitafutwa na kukamatwa,” alisema.

 

Kwa mujibu wa Kamanda Katabazi, uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

 

Akizungumzia tukio hilo, mmoja kati ya shuhuda wa tukio hilo, Hassan Juma, alisema Batezi na Ngowo, walikuwa wanakunywa pombe na msichana huyo eneo la Songambele na baadaye walikwenda kulala naye eneo la Kazamoyo nje kidogo ya Songambele.

 

Shuhuda huyo alidai kuwa watuhumiwa hao walishirikiana na watu wengine kumfanyia mhudumu huyo unyama huo kwa kumbaka, kumlawiti na kisha kumwingizia chupa ya bia kwenye sehemu ya haja kubwa.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mirerani, Dk. Deogratius Mazengo, alipoulizwa na Nipashe kuhusu majeruhi huyo, alithibitisha kutibiwa kituoni hapo baada ya kupelekwa na polisi akiwa na fomu namba tatu ya polisi (PF3) inayomruhusu kutibiwa.

Habari Kubwa