Mbaroni kwa madai ya kumuua ‘shamba boi’, mwili wake kuufukia

05Aug 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mbaroni kwa madai ya kumuua ‘shamba boi’, mwili wake kuufukia

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu wanne akiwamo mwanamke kwa tuhuma za mauaji ya mchunga mifugo, Shabani Mbalali (20), mkazi wa Chamanzi ambaye baada ya kumuua walimfukia na kuiba mbuzi watano.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro, alisema kijana huyo aliuawa na watu wasiofahamika Jumamosi iliyopita, eneo la Chamazi Vigoa akiwa machungani.

“Akiwa anachunga mbuzi eneo hilo, watu wasiofahamika walimuua na kuiba mbuzi watano na kisha mwili wake kuufukia kwenye shimo,” alisema.

Muliro alisema katika ufuatiliaji walikamatwa watu wanne ambao ni Anold Kavishe (36) mkazi wa Maji Matitu, Justine Joseph (32) mkazi wa Kisewe, Selemani Hamisi (39) mkazi wa Chamazi na Joyce John (38) mkazi wa Maji Matitu.

Katika tukio lingine, Kamanda Muliro alisema wanawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kutishia kwa bastola wanazozimiliki.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Isack Willy (44), maarufu Wambura mkazi wa Sinza E, Rashid Mshana (36) na Mussa Mshana (39) wote wakazi wa Mwenge na Ibrahim Shaibu (52) mkazi wa Kinyerezi.

Alisema mtuhumiwa Willy akiwa baa iitwayo 99 Vibes maeneo ya Sinza, alitoa silaha aina ya Browning na kudaiwa kutishia watu akiwa amelewa.

“Mtuhumiwa Rashid alionekana kwenye ‘video clip’ iliyosambaa kwenye mtandao wa kijamii akitishia kwa silaha aina ya Browning. Tulifanya upelelezi na kumkamata na silaha yake ikiwa na risasi 10 ndani ya magazine. Silaha hiyo  inamilikiwa na kaka yake Mussa,” alisema.

Alisema Mussa anatuhumiwa kwa kosa la uzembe kwa kumwachia silaha mdogo wake ambaye ni Rashid aliyejirekodi akitishia watu na kudaiwa kutuma mtandaoni.

“Agosti Mosi jioni maeneo ya Vijibweni Kigamboni mtuhumiwa Ibrahim alimtishia kumuua kwa silaha jirani yake aliyefahamika kwa jina la Chacha Mwita walipokuwa wakigombea mipaka ya kiwanja. Alikamatwa na bastola aina ya Luger ikiwa na risasi sita,” alisema.

Kamanda alisema silaha hizo zinashikiliwa wakati utaratibu wa kisheria ukifuata ikiwa ni pamoja na kuwafutia umiliki wake.

“Unapewa silaha alafu unaanza kuitoa ovyo ovyo pasipo sababu, kupewa silaha unataka watu wajue una silaha pasipo sababu ya msingi, katika mazingira ambayo hayaruhusiwi ikibainika tunafuata taratibu kama hawa, hizi si silaha za maonyesho kwenye maeneo yenu,” alisema.

Alisema wanaendelea kufuatilia kwa ukaribu na halitasita kuwanyang’anya wakiwamo walevi wataosababisha silaha zikaingia mikononi mwa wahalifu.