Mbaroni kwa mauaji ya mtoto wake

29Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Babati
Nipashe
Mbaroni kwa mauaji ya mtoto wake

Mkazi wa Kijiji cha Bassotu Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara, Elibariki Shaban (50) anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wake kwa kumpiga.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna msaidizi Maresone Mwakyoma, amesema tukio hilo limetokea Oktoba 26 mwaka huu kwenye kijiji cha Bassotu.

Kamanda Mwakyoma amesema Shaban anadaiwa kumpiga mtoto wake, Amos Elibariki (25) kwa deki usoni, makofi na mateke na kufariki dunia wakati akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Haydom.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni baba kumpiga mtoto wake baada ya kubishana kwenye mambo yao ya kifamilia na mzee huyo kuchukia.

Amesema Shaban alipohojiwa na polisi sababu za kumpiga mwanaye alisema alimpiga kwa kuwa mtoto huyo alimtukana na yeye hasira ilimpanda na kuamua kumuadhibu.

"Amos aliaga dunia wakati wakimkimbizwa kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Haydom ili akapatiwe matibabu," amesema Mwakyoma.

Habari Kubwa