Mbaroni kwa tuhuma uhalifu wa mtandao

13Sep 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mbaroni kwa tuhuma uhalifu wa mtandao

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu tisa wakiwamo raia saba wa kigeni kwa tuhuma za uhalifu wa mtandao.

Kati yao, wawili wanatuhumiwa kujifanya maofisa wa usalama wa taifa na polisi na kutapeli Sh. milioni 35.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, alisema watuhumiwa hao walikamatwa kupitia msako maalum uliofanywa kwa miezi miwili kuanzia Agosti.

Aliwataja raia hao na nchi walizotoka kwenye mabano kuwa ni Adewale Oyedes (Nigeria), Ibrahim Darbey, Prince Tito na Cream Elias (wote Liberia), Basube Dominic (DRC), Sibongile Arhur (Afrika Kusini) na Baljit Singh (India).

Kamanda Mambosasa alisema raia hao wenye umri kati ya miaka 28 na 46, walikamatwa katika maeneo mbalimbali jijini kwa tuhuma za utapeli na wizi kwa njia ya mtandao.

“Baada ya mahojiano, watuhumiwa hawa walikiri kujipatia Sh. milioni 10 kwa njia ya udanganyifu kupitia mtandao na baadhi ya fedha hizo zilitumika kuanzisha duka la vinywaji vya pombe kali eneo la Tangi Bovu Mbezi Beach, tumevitia mbaroni, walinunua gari aina ya Toyota Mark, luninga mbili na magodoro, yote ni matokeo ya zao la uhalifu wanaoufanya,” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema watuhumiwa hao walikiri kujihusisha na wizi kwenye taasisi za kifedha na waliingia nchini kwa njia tofauti na baada ya kufika Tanzania, walikaribishwa na watanzania.

“Wapo Watanzania ambao wamewakaribisha kama waume zao ambao wameendelea kuishi nao, lakini kipato wanachopata ni cha kupitia wizi kwenye mitandao,” alisema.

Alisema watuhumiwa hao wamekiri kufanya uhalifu huo katika nchi nyingine barani Afrika ambazo walizitaja kwenye mahojiano kuwa ni Malawi, Uganda, Kenya na Afrika Kusini.

“Nitoe onyo kwa raia wa kigeni kuwa Tanzania ni nchi yenye sheria zake, tunawapenda wageni anayetaka kuja nchini milango ipo wazi kwa kufuata taratibu zote, akiwapo nchini ana jukumu la kufuata sheria za nchi.

“Watuhumiwa hawa wameingia kwa nia ya kufanya uhalifu, nchini kwao uhalifu hautakiwi, sasa wanakuja Tanzania, hakuna atakayebaki salama kwa wale wanaokuja kwa lengo la kutenda uhalifu. Walichokipanda ndicho wanachokivuna," alionya.

Kamanda Mambosasa alisema katika msako huo, pia walikamata Watanzania wawili kwa kujifanya maofisa usalama wa taifa na polisi.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Patrick Tarimo (32), mkazi wa Mwenge ambaye inadaiwa amekuwa akijitambulisha kama Ofisa Usalama wa Taifa na Castory Wambura (57), mkazi wa Kibamba anayedaiwa kujifanya ni askari polisi.

“Agosti 10 mwaka huu, Tarimo alijipatia Sh. milioni 20 kutoka kwa raia wa kigeni ambaye alimkamata na kujitambulisha kuwa ni Ofisa Usalama wa Taifa na kufanikiwa kujipatia fedha hizo.

“Agosti 21, mwaka huu mtuhumiwa Wambura alitapeli kiasi cha Sh. milioni 15 kutoka kwa wafanyabiashara watano wa sokoni Kariakoo baada ya kujitambulisha ni Ofisa wa Polisi na Mamlaka ya Mapato (TRA)," alisema.

Habari Kubwa