Mbaroni kwa tuhuma za kumbaka mtoto

26Jan 2017
Rose Jacob
MWANZA
Nipashe
Mbaroni kwa tuhuma za kumbaka mtoto

JESHI la Polisi mkoani Mwanza, linamshikilia Petro Magayane (22) kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka mitano na kumsababishia maumivu.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi, alisema tukio hilo lilitokea Januari 23, mwaka huu saa 20:00 usiku katika Kijiji cha Igombe `A' Kata ya Bugogwa Wilaya ya Ilemela.

Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa Magesa akiwa amelewa, alifika maeneo ya nyumbani anapoishi mtoto huyo kisha akamtuma dukani eneo la Mwaloni Igombe.

Hata hivyo, alisema baada ya muda mchache kupita, mtuhumiwa huyo alimfuata mtoto dukani na kumbaka.
Alisema raia wema walitoa taarifa polisi ambao walikwenda eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa.

Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa polisi na uchunguzi ukikamilika, atafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.

Kamanda Msangi alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini wakati wote na watoto ili kuwaepusha na watu wenye nia mbaya dhidi yao.

Habari Kubwa