Mbaroni tuhuma  mauaji wanawake watatu 

19May 2022
Neema Hussein
KATAVI
Nipashe
Mbaroni tuhuma  mauaji wanawake watatu 

JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi, linamshikilia Richard Michael (25), mkazi wa mtaa wa Shanwe, Manispaa ya Mpanda kwa tuhuma za mauaji ya wanawake watatu yaliyofanyika mwezi uliopita kwa nyakati tofauti katika mtaa wa Ilembo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Sylvester Ibrahim.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Sylvester Ibrahim, alisema jana akizungumza na waandishi wa habari baada ya matukio hayo polisi walifanya msako na kumkamata Crispin John akiwa na simu ambayo ilipokwa kwa marehemu Zainab Abdala baada ya kuuawa Aprili 2, mwaka huu.

 

Alisema mtuhumiwa baada ya kuhojiwa, alikili kufanya mauaji ya wanawake hao kisha kuwanyang'anya vitu mbalimbali alivyowakuta navyo kama vile simu, mikoba, pesa kisha miili yao kuitelekeza vichakani na kwenye mashamba ya mahindi.

 

Alisema mtuhumiwa baada ya kukiri, aliwaongoza viongozi mbalimbali wa mtaa, Jeshi la Polisi na baadhi ya familia za marehemu kuonyesha maeneo yote aliyofanyia ukatili huo.

 

Baada ya kufika katika eneo mojawapo, alisema walikuta viatu vya marehemu ambavyo vilijulikana na ndugu.

 

Kamanda Ibrahim alisema mtuhumiwa wakati akiliongoza jeshi hilo kwenda eneo la tukio, alilegeza pingu na kisha kukimbia, hivyo kusababisha askari kupiga risasi mbili hewani kumtaka asimame.

 

Alisema mtuhumiwa hakufanya hivyo ndipo walimjeruhi kwa risasi maeneo ya mgongoni na wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Katavi, alifariki dunia.

Habari Kubwa