Mbaroni tuhuma kukutwa na vifaa tiba bila ya vibali

02Apr 2020
Idda Mushi
Morogoro
Nipashe
Mbaroni tuhuma kukutwa na vifaa tiba bila ya vibali

JESHI la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kupatikana na dawa za binadamu na vifaa tiba bila kibali huku wakidaiwa kutoa huduma za kitabibu kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Wilbroad Mutafungwa, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti ya mkoa wa Morogoro wakati wa doria za askari baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Tukio la kwanza, alisema lilitokea katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro ambako Barnabas Mayunga (32), mkazi wa Kihonda kwa Mkomola, Manispaa ya Morogoro alikamatwa na dawa mbalimbali za binadamu pamoja na vifaa tiba vingine vikiwa na nembo ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na vifaa hivyo vikiwa katika gari lake lenye namba za usajili T 394 DKP aina ya Toyota Harrier na vingine akiwa navyo nyumbani kwake bila kibali.

Mutafungwa alivitaja vifaa vilivyokamatwa kuwa ni ‘cotton wool’, fomu ya bima ya afya moja isiyojazwa, dripu sita za MSD, Ketavit 50, lignocain injection moja, sare moja ya rangi ya kijani, kitambulisho cha mpigakura, glovu mbili, folic Acid dozi moja, Chromit Catgut 15, Eocost Plastnne na Calvista mbili.

Vifaa vingine alivyokamatwa navyo ni vitabu vitano vya matibabu ya wagonjwa, fomu nne za matibabu, mkasi.

Vingine amevitaja kwa majina ya heine moja, Feiya moja, Kiboksi cha huduma ya kwanza, Gentremycine 10, Epirucks maboksi mawili, mpira mmoja wa kupitishia mkojo, Acne free mbili, Oracure moja, Irefone Gery 01, Amoxyline saba, Lamopazzle boksi moja, Nirixone Aoana Phamaecetical maboksi mtano, Pantacid moja, Lignocare moja pamoja na Ketajet.

Vingine, kwa mujibu wa Mutafungwa, ni mabomba 22 ya sindano, mashine ya kupima shinikizo la damu, nailoni moja ya 60 MG, Artesun moja, boksi moja la Panadol, Aroxicam moja, D-Artep moja, Safeteram moja na Haema cap moja.

Kamanda Mutafungwa akabainisha kuwa, Polisi wanaendelea kuchunguza kwa kina taaluma ya mtuhumiwa huyo kwa madai kuwa bado ameendelea kujitambulisha kama daktari katika maeneo mbalimbali.

“Awali alikuwa akifanya kazi hospitali ya mkoa na akaondolewa, kwa hiyo bado haieleweki aliingiaje hapo hospitalini na amesomea wapi taaluma hiyo ya udaktari. Kikikubwa zaidi ni kuwa na hivi vifaa tiba na dawa ambazo zingine zina nembo ya MSD bila kuwa na kibali,” alisema.

Mutafungwa alisema tukio lingine linamhusisha Daniel Nelson (28) mkazi wa Kitongoji cha Minjenja, Wilaya ya Gairo, aliyekamatwa akiwa na vifaa vya matibabu ya binadamu anavyomiliki nyumbani kwake bila kibali.

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na Canula, MVA-Set and Tube, Stetoscope, mashine ya kupimia shinikizo la damu, koti la kitabibu, Metal Tray, Mayo scissor, speculam, penguinsucker, toothed, artery force na sponge holding force.

SACP Mutafungwa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya awali kukamatwa kwa tuhuma za kumtorosha binti kutoka kwenye himaya ya wazazi wake na alipokwenda kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake, alikamatwa akiwa na vifaa hivyo.

Inadaiwa mtuhumiwa awali alikuwa akifanya kazi kwenye hospitali moja ya misheni katika idara ya maabara na baada ya kuacha kazi, ikadaiwa akawa anaendelea kutoa huduma za matibabu ya binadamu kienyeji na kwa uficho nyumbani kwake.

Kamanda huyo wa Polisi alisema watuhumiwa hao wote wawili bado tuhuma zao zinachunguzwa na baadaye watafikishwa mahakamani.

Habari Kubwa