Mbaroni tuhuma za mauaji mgodini

11Jul 2020
Neema Sawaka
Kahama
Nipashe
Mbaroni tuhuma za mauaji mgodini

MKUU wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi, Kamishna Liberatus Sabas, amezitaka mamlaka zinazoshugulikia utoaji wa nyaraka na vibali vya kusafirisha mchanga wa dhahabu, kujiridhisha kuhusu uhalali wa mchanga huo kwa kufika kwenye eneo unakotolewa.

Vilevile, amesema watu 13 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watu wanne eneo la uchenjuaji dhahabu wilayani Kahama mwishoni mwa mwezi uliopita.

Mihayo Msikhela amesema kuna haja wahusika kujiridhisha unakotoka mchanga huo na kumbaini mmiliki halali wa eneo au mchanga husika, ili kueupuka kutoa vibali kwa mchanga uliopatikana kwa njia ya uhalifu na kuikosesha mapato serikali.

Alitoa rai hiyo juzi alipowasilisha taarifa kuhusu tukio la mauaji ya watu wanne yaliyofanyika katika Mgodi wa Wachimbaji Wadogo Tambalale Na. 4 ulioko Kijiji cha Wisolele, Kata ya Segese wilayani Kahama.

Msikhela alisema kuwa katika tukio hilo lililotokea Juni 30, mwaka huu majira ya saa mbili usiku kwenye eneo la kuchenjua dhahabu, watu wanne waliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya kichwani na watu wasiojulikana.

Kiongozi huyo aliwataja waliouawa katika tukio hilo kuwa ni: Juma Jigwasanya (42), mlinzi wa Kampuni ya Sekepa na mkazi wa Nundu, Nyang’hwale; Lusajo Mwamasangula (31), mlinzi wa Kampuni ya Sekepa na mkazi wa Tine; Raphael Mapinduzi (27), mwendesha mitambo huo na mkazi wa Katoro, Geita; na Daniel William Mapunda (25), msimamizi wa mtambo na mkazi wa Geita.

Alisema kuwa katika tukio hilo, Exavery Maulid (21), mwendesha mitambo, alinusurika kifo baada ya kujeruhiwa kwa kugongwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani kisha kuwekwa pamoja na miili ya marehemu, wahusika wakiamini tayari alikuwa ameshapoteza maisha.

Alisema kuwa baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi kwa kushirikina na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi, walianza msako wa kuwatafuta wahalifu hao na kufanikiwa kuwakamata wahalifu 13 wakiwa na vielelezo mbalimbali na kuongeza kuwa baada ya upelelezi kukamilika, watafikishwa mahakamani.

Alisema kuwa uchunguzi wao umebaini kuna kundi la uhalifu lililopanga mpango huo wa mauaji na lilitekeleza uhalifu na mauaji hayo kisha kusafirisha na kuhifadhi mzigo huo baada ya wizi kufanyika.

Alibainisha kuwa baadhi ya vielelezo vilivyokamatwa ni mchanga wenye Carbon iliyonasa dhahabu, viroba saba ulioibwa katika mtambo siku ya tukio ukiwa na uzito wa kilogramu 385.34, makapi ya mchanga wenye kaboni ukiwa na uzito wa kilogramu 465.76 uliokutwa umefichwa katika nyumba ya mmoja wa watuhumiwa ukiwa pamoja na viroba saba vya mchanga wenye kaboni iliyoibwa siku ya tukio.

Vielelevyo vingine ni pikipiki tano ikiwamo iliyotumika kubeba huo mzigo na nyingine moja ambayo mtuhumiwa alikimbia na kuitelekeza kwenye nyumba aliyokuwa akilinda viroba vya Carbon iliyokuwa imeibwa.

Vingine bunduki aina ya shortgun yenye namba 9025817 iliyoporwa kwa mlinzi mmoja wapo aliyeuawa siku ya tukio ikiwa na risasi mbili na baadaye kutelekezwa umbali wa mita 400 toka eneo la tukio. Pia panga lenye vimelea vya damu.

Habari Kubwa