Mbaroni wakituhumiwa kubaka mtoto kwa zamu

16Oct 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Mbaroni wakituhumiwa kubaka mtoto kwa zamu

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, linawashikilia vijana wawili, wakazi wa mkoani hapa kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka sita kwa zamu.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba, akitoa taarifa hiyo jana kwa vyombo vya habari, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 12, mwaka huu majira ya saa tatu kasorobo usiku.

Alisema watuhumiwa hao (majina yao yanahifadhiwa kutokana na kuwa na umri chini ya miaka 18), walimlaghai mtoto huyo kuwa watamnunulia pipi pamoja na kumpatia hela, na kisha kumpeleka vichakani nyuma ya nyumba yao na kuanza kumbaka kwa zamu.

"Tukio la kubakwa kwa mtoto huyu liligunduliwa na mama yake mzazi (jina limehifadhiwa), ambaye alikuwa akimtafuta mwanawe na kumuona akiwa ameumia sehemu za siri, ndipo akatoa taarifa polisi," alisema Magiligimba.

Alisema chanzo cha mtoto huyo kubakwa ni tamaa za kingono na kwamba upelelezi ukikamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani, ili kuchukuliwa hatua kali zaidi za kisheria.

Pia, kamanda alitoa wito kwa wazazi na walezi mkoani humo, kuendelea kutoa taarifa za ukatili, ili wahusika wachukuliwe hatua na kukomesha vitendo hivyo.

Habari Kubwa